• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
WARUI: Serikali iharakishe utoaji chanjo kuokoa sekta ya elimu

WARUI: Serikali iharakishe utoaji chanjo kuokoa sekta ya elimu

Na WANTO WARUI

INGAWA kurejea kwa masomo katika shule na vyuo vya elimu kulileta matumaini ya kuendeleza elimu baada ya kufungwa kwa muda kutokana na ugonjwa wa Covid-19, bado kuna kasoro kubwa sana katika sekta hii.

Elimu inayotolewa kwa sasa haijakamilika kwani kuna mambo kadha ambayo yanazuia kutolewa kwa elimu kikamilifu.

Kalenda ya shule ambayo ilitolewa na Wizara ya Elimu imepunguza mihula ya masomo hivi kwamba kila muhula umepungua kwa mwezi mzima au zaidi.

Licha ya hayo, walimu wanatakiwa wakamilishe silabasi ya kila darasa kwa muda huo mfupi sana jambo ambalo linatatiza.

Hili linawaacha walimu na wanafunzi waking’ang’ana kufikia angalau robo tatu ya mahitaji ya silabasi.Aidha, elimu haiwezi kukamilika pasipo shughuli za michezo shuleni ambazo humchangamsha mwanafunzi na kumwezesha kunyoosha viungo vya mwili na ubongo.

Tangu kuingia nchini kwa Covid-19, mashindano ya michezo ya shule na vyuo yalisimamishwa hivyo basi kuzuia kutangamana kwa wanafunzi.

Kutangamana huku kulikuwa ni muhimu sana kwa wanafunzi kwani kulisaidia kutekeleza malengo muhimu ya elimu kama vile mshikamano wa kijamii na mwingiliano wa kitabaka.

Aidha, kuna sehemu nyingine muhimu sana za elimu ambazo haziendelezwi.

Hizi ni pamoja na tamasha za muziki za shule na vyuo. Ni katika tamasha hizi za muziki ambapo nchi huweza kutoa watu mahiri na wenye talanta mbalimbali.

Ukariri wa mashairi na nyimbo ni mojawapo ya njia ambazo hupanua bongo za wanafunzi na kuwawezesha kuelewa mambo vyema na kwa upana.

Michezo ya kuigiza pia ni sehemu nyingine muhimu katika fani ya elimu ambayo huwawezesha wanafunzi kutambua masuala kadhaa katika jamii zetu.

Mtaala

Kuna Mtaala mpya wa Elimu, CBC, ambao unawahitaji wanafunzi wasome kwa pamoja katika makundi kwa kushirikiana.

Mambo haya yote na mengine mengi yamelemaza elimu kwa kiasi kikubwa sana hivi kwamba elimu inayoendelea sasa shuleni haijafikia viwango hitajika na wanafunzi wataathiriwa sana siku za baadaye.

Hii ndiyo sababu kuna haja kubwa sana kwa serikali kupambanukiwa zaidi na masuala haya ya elimu na mambo mengine muhimu yanayodidimiza uchumi wa taifa.

Wizara ya Elimu inastahili kufanya hima kuhakikisha kuwa serikali inafanya kila iwezalo usiku na mchana kuwezesha wanachi wote wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 ili iwe rahisi kurejesha elimu katika viwango vinavyostahili.

Kufikia sasa, idadi ya wananchi ambao wamepata chanjo ingali chini ya milioni tatu!

You can share this post!

WASONGA: Raia wasibebeshwe mzigo wa kulinda mali ya wakuu

Ujerumani wakomoa Armenia 6-0 na kutua kileleni mwa Kundi J...