• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
KINA CHA FIKIRA: Wakati ni sasa, tumia leo kutengeneza kesho yako

KINA CHA FIKIRA: Wakati ni sasa, tumia leo kutengeneza kesho yako

Na WALLAH BIN WALLAH

SAFARI ya kesho hupangwa leo. Usipoipanga safari ya kesho leo, kesho itakapofika, safari yenyewe itakupangua!

Ni vizuri kuwa na mpangilio wa kujipangia maisha mapema bila kufanya ajizi ajizi ambayo siku zote ni nyumba ya njaa!

Matatizo na majuto makubwa husababishwa na wanadamu wasiotumia muda wao kujiandaa mapema kuyatengeneza maisha yao ya baadaye!

Kila mtu anapaswa kuutumia wakati wake kwa makini! Tusiupoteze wakati ndipo tuje kuulilia kama mtu anayeyalilia maziwa yakishamwagika!

Leo ndiyo siku muhimu ya kujiandaa kuyakabili maisha ya kesho! Hiyo ndiyo sababu mkulima mwerevu hulitayarisha shamba lake mapema; hupanda mbegu mapema; hupalilia, huvuna mazao vizuri na kuyatunza vizuri!

Dadisi uone! Utagundua kwamba siri ya mafanikio maishani ni kuanza shughuli na majukumu mapema bila ngoja ngoja za kuumiza matumbo!

Maisha ya kesho hutengenezwa leo! Ujana wa leo ndio uzee wa kesho! Masomo ya leo shuleni ndiyo elimu ya kesho itakayomsaidia mtu kupata kazi!

Halafu kazi italeta mshahara wa kutumia katika maisha yajayo! Huo ndio mpangilio wa mafanikio katika maisha!Mtu yeyote asiyetumia leo yake vizuri kwa akili na busara, anavuruga na kuibomoa kesho yake!

Leo ni leo, msema kesho bila ya kuitumia leo yake vizuri ni mwongo! Wakati ndio huu!! Tumia wakati ulio nao kuyatengeneza maisha mema ya baadaye!

Uzembe

Linalowezekana leo lisingoje kesho. Tabia ya kujivutavuta kufikiria kuhusu maisha ya baadaye ndiyo chanzo cha shida na majuto maishani!

Uvivu na uzembe wetu ndio umaskini na ufukara wetu maishani. Kumekucha! Kila mtu aamke akae macho afikirie kesho yake!

Tumia leo yako kuitengeneza kesho yako! Ukiwa wewe ni mkulima, usiyauze mazao yote uliyovuna na kubaki bila akiba kana kwamba hujui kesho kuna njaa! Utakula nini? Ukiwa wewe ni mfanyakazi, Mungu alikujalia ukaajiriwa ulipokuwa kijana, halafu miaka yote umekuwa ukilipwa mshahara na kuzitumia pesa zote mpaka senti ya mwisho bila kuweka akiba ya maisha ya baadaye, utajivunia akili gani?

Utaishi vipi uzeeni utakapostaafu

Ukichunguza mambo vizuri utagundua kwamba hata wanyamapori kama fisi na nyani huweka akiba! Nyani wakivamia shamba la mahindi, wanapotoka au wanapofukuzwa, lazima wabebe mahindi akiba ya kula baadaye!

Fisi na ulafi wake, akishakula mzoga akashiba, utamwona akitembea na mfupa mdomoni kupeleka pangoni mwake kuweka akiba ya kuguguna baadaye!

Ndugu wapenzi, leo ndiyo siku ya kujitengenezea kesho yako! Wakati ndio huu! Tumia leo yako kuijenga kesho yako! Usiseme sikukwambia!

You can share this post!

Wakazi wateketeza lori lililogonga na kuua mwanafunzi

Cheruiyot tayari kuonyesha bingwa wa Olimpiki Ingebrigtsen...