• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
AKILIMALI: Punda ni ofisi yake; anawauza kwa wanaosaka mbinu ya usafiri

AKILIMALI: Punda ni ofisi yake; anawauza kwa wanaosaka mbinu ya usafiri

Na RICHARD MAOSI

TAKWIMU zinaonyesha kuwa punda hutumika kubeba mizigo mizito mashinani, hususan katika maeneo ambayo miundo misingi ya barabara ni duni.

Aidha, wasimamizi wa vichinjio vya punda wamelaumiwa kwa kuhatarisha maisha ya wanyama hawa kupitia biashara ya viungo vyao, huku wezi wa punda wakivuna sehemu ambayo hawakupanda.

Hata hivyo, kwa mama Teresia Mumbi, mkulima kutoka kijiji cha Kwa Njaga, Kaunti ya Nyandarua, punda wamekuwa ni ofisi yake.

Anasema ukulima na uchukuzi kwa Wakenya wengi unategemea miundo msingi bora ya usafiri, ndio maana wakulima wengi mashinani wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata hasara mazao yao yanapochelewa kufika sokoni kwa wakati.

Kulingana naye ni jambo ambalo limewafanya kuwekeza kwenye mradi wa kufanya biashara ya punda ambapo mara nyingi huuzwa kati ya Sh20,000-25,000.

Ingawa wakulima wengi kutoka Kaunti ya Nyandarua wanakuza viazi, maharagwe, mihogo na mahindi, Mumbi anasema kuwa hajutii kujikita kwenye mradi huu, ambao umetengeneza nafasi nyingi za ajira na kurahisisha usafiri.

Kulingana naye, anaungama kuwa endapo wakulima watawapatia punda mafundisho mwafaka jinsi ya kuishi na mifugo, wanaweza kukaa na wanyama wengine kama vile kondoo, mbuzi au ng’ombe na hata kuwapatia ulinzi.

Punda katika kijiji cha Kwa Njaga, Kaunti ya Nyandarua. Wakulima wamekuja na mbinu mwafaka ya kufanikisha ufugaji kwa kukata kwato, kuwapatia chanjo na kuwatengenezea mazingira mazuri. Picha/Richard Maosi

Isitoshe alieleza kuwa ni wanyama ambao wanaweza kujitafutia malisho na kudumu katika mazingira magumu yenye joto au baridi kali.

Kwa upande mwingine wakulima wengi kutoka Nyandarua ambao wanategemea punda, wamekuja na mbinu ya kuboresha ufugaji wa punda baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa wataalam na wanaharakati wanaotetea haki za punda.

“Kwanza punda wanafaa kubebeshwa mizigo kulingana na uwezo wao, aidha wanahitaji wakati wa kutosha kupata mapumziko,” akasema.

Mumbi alifichulia Akilimali kuwa yeye huhakikisha kuwa punda wake wanapata maji ya kutosha wakati wowote ambao huwa hawafanyi kazi.

Vilevile, amewatengenezea punda wake watatu banda nzuri kuwakinga dhidi ya mvua, baridi kali au jua.

Alifichua kuwa kila siku akiamka huhakikisha kuwa punda wake wamelishwa vyema na kuwapangusa kwato kabla ya kurejelea shughuli za siku kusafirisha mazao kutoka shambani hadi sokoni.

Baada ya kufanya vibarua sehemu mbalimbali miaka ya awali, aliamua kutafuta mbinu mbadala ya kujiendeleza kimaisha ambapo alinunua mtoto wa punda na kumtunza hadi akakomaa.

Hapo alianza kutengeneza hela kwa kufanya vibarua kijijini kama vile kubeba mizigo, au kukodisha kwa wafanyabiashara wengine na hata kubebea maji kutoka mtoni.

Ikumbukwe kuwa kijiji cha Kwa Njaga kina miundo msingi duni ambapo miinuko na mabonde hufanya nyingi ya sehemu zisiweze kupitika hasa wakati wa mvua nyingi.

Alieleza kuwa imekuwa ni nafuu kwa vijana wengi na akina mama ambao walikuwa wamezoea kushinda mtaani, kwa sababu punda wametoa fursa ya kutengeneza nafasi nyingi za kazi.

“Barabara nyingi hapa hazipitiki, jambo ambalo limekuwa likiwafanya wakulima kukadiria hasara kubwa mazao yao yanapochelewa kufika sokoni,” akasema.

Alieleza kuwa changamoto za wakulima wa matunda na mboga zilikuwa nyingi huku wengi wao wakikosa kujua namna ya kuhifadhi mazao ya shambani mara tu baada ya kuvuna.

Aliongezea kuwa kinyume na awali watu wengi hawakuwa wakizingatia maslahi ya punda kama vile kuwaacha wajitafutie vyakula na kuishi kwenye mazingira duni.

Matunzo ya punda

Beth Kuria ambaye ni mwekahazina kutoka Shirika la Muungano wa Wamiliki wa Punda nchini (ADOK), aliambia Akilimali kuwa pana haja ya serikali kutilia mkazo suala la kuwahifadhi punda kwenye mazingira mazuri.

Alieleza kuwa wafugaji wengi wameshindwa kuwapatia punda malazi mazuri na lishe bora, jambo ambalo amelitaja kuma kuwakosesha haki zao za kimsingi.

Alieleza kuwa kama wanyama wengine punda wanahitaji kupatiwa lishe nzuri na chanjo kila mara, hii ikiwa na pamoja na kuwafanyia huduma za kukata kwato na kuwawekea matandiko mazuri wakati wa kubebea mizigo ili ngozi yao isije ikachujuka.

Aliongezea kuwa akinamama wengi wanaokaa mashambani wanategemea punda kufanyia kila kitu kama vile kusafirisha viazi hadi sokoni na hata kuwabebea maji kutoka mtoni.

You can share this post!

Wanasoka wa Chelsea na Bayern Munich wabeba Ujerumani dhidi...

AKILIMALI: Huzifikirii sana chupa za plastiki ila kwake ni...