• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Waiguru adai ni vigumu kuchaguliwa kupitia Jubilee

Waiguru adai ni vigumu kuchaguliwa kupitia Jubilee

Na GEORGE MUNENE

GAVANA wa Kirinyaga, Anne Waiguru kwa mara ya kwanza amekiri hadharani kuwa, atakuwa na kibarua kigumu kutetea kiti chake kupitia chama cha Jubilee katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, Bi Waiguru alisema chama hicho kwa sasa hakishabikiwi mno Mlima Kenya kama zamani na anayelenga kukitumia kuwania kiti chochote huenda akashindwa vibaya uchaguzini.

“Ukweli ni kwamba, kutetea kiti changu kwa tiketi ya Jubilee iwapo hata uchaguzi ungeandaliwa leo, itakuwa vigumu. Huo ndio ukweli,” akasema Bi Waiguru huku kauli yake ikifasiriwa kuwa huenda ana nia ya kujiunga na kambi ya Naibu Rais Dkt William Ruto.

Hata hivyo, mpinzani wake mkuu Wangui Ngirici tayari yuko kwenye mrengo wa Hasla.

Bi Waiguru alikariri kuwa wakazi wengi wa Kirinyaga hawajaridhishwa na jinsi ambavyo chama kimeendeshwa kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, alitetea utendakazi wake, akishikilia kuwa ametimiza miradi mingi ya maendeleo na hilo haliwezi kuchangia kushindwa kwake debeni.

Alisisitiza kuwa Jubilee inahitaji mageuzi makubwa ya uongozi na bado anatafakari kuhusu chama atakachotumia 2022 kutetea kiti cha ugavana kisha awatangazie wananchi baadaye.

Mnamo 2017, umaarufu wake ulichangia ushindi mkubwa na kuchangia kumbandua aliyekuwa Gavana Joseph Ndathi uongozini.

Akizungumza katika eneobunge la Gichugu baada ya kukagua miradi ya maendeleo wikendi, Bi Waiguru alisema atakumbatia chama ambacho wananchi watamshauri ajiunge nacho.

“Uamuzi wangu utategemea kile wananchi walionipigia kura 2017 wanataka. Wao ndio wana kura na siwezi kuwakaidi,” alisema.

You can share this post!

TAHARIRI: Ahadi ya kazi kwa vijana iko wapi?

Polo auguza nyeti kisiri nyumbani