• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
ULIMBWENDE: Njia rahisi za kutunza ngozi yako wikendi

ULIMBWENDE: Njia rahisi za kutunza ngozi yako wikendi

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KWA wengi, wikendi ni muda mzuri wa kuhakikisha mambo yanaenda sawa katika miili yetu na hata majumbani, ni muda wa mapumziko ambao tunatumia kusafisha nyumba, mavazi, na hata kufanya usafi wa mwili.

Siku za wiki huwa tunafanya mambo kwa haraka na aghalabu hatuna muda wa kutosha kujijali vizuri.

Hivyo basi, wikendi ndio muda maalum wa kusafisha nywele, kucha bila kusahau kutunza ngozi.

Pata usingizi wa kutosha

Usingizi ni mzuri katika kutunza ngozi yako. Ni muhimu mtu kulala kwa angalau muda wa saa nane au zaidi ili kupumzika vya kutosha.

Tumia wikendi kulala kwa kipindi cha saa nane au zaidi kufidia muda uliopotea kwa wewe kufanya kazi kupitiliza. Kwa kufanya hivyo, mwili na ngozi yako inapata matunzo mema.

Faida za mtu kupata usingizi wa kutosha

  • hupunguza mikunjo katika ngozi
  • ngozi hujikarabati yenyewe usiku
  • vipodozi au mafuta yanapata muda mwingi wa kutengeneza ngozi
  • ngozi inakuwa yenye afya

Fanya ‘Facial’

Ikiwa kwenda kufanyia saluni ni ghali, basi unaweza kufanya facial nyumbani.

Ima uwe unatumia bidhaa za kununua au za asili hapo nyumbani, hakikisha unafanya facial ili kusafisha ngozi yako na kuiacha katika hali nzuri.

Facial husaidia kuifanya ngozi iwe safi na yenye afya. Unaweza kuanza na kusafisha ngozi ukitumia cleanser. Osha na kisha paka maski yako. Kaa nayo kwa muda unaofaa na uondoe kisha weka unyevu – moisturize – ngozi yako.

Kuwa bila vipodozi

Wiki nzima inawezekana ukawa unapaka vipodozi wakati wa shughuli zako za kikazi hivyo ukawa umekosa kabisa muda na hata ukajipata umepanda nayo kitandani na kulala hivyo!

Wikendi ni muda bora zaidi wa kuacha ngozi yako ipumue iepukane na kemikali ambazo huwa umejipaka wiki nzima. Unaweza kuiacha ngozi yako ikiwa bila vipodozi kwa saa chache kabla ya kupaka tena.

You can share this post!

Sheria maalum zawekwa kudhibiti sekta ya ujenzi Kiambu

AFYA: Umuhimu wa mtu kula chakula kwa uwiano unaotakiwa