• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Mtindo bora wa maisha

Mtindo bora wa maisha

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Fanya mazoezi

Zoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kupumua kwa kasi. Kiwango kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tano kwa wiki.

Faida za mazoezi na kujishughulisha ni:

  • kudhibiti sukari na mafuta yaliyozidi mwilini
  • kuepusha shinikizo kubwa la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani
  • kuboresha mzunguko wa damu mwilini kwa afya ya mifupa na misuli
  • kujenga misuli
  • kupunguza unene na uzani
  • kupunguza mawazo na kuwezesha usingizi mnono

Mifano ya kujishughulisha

  • kusafisha nyumba na kufanya kazi nyingine za nyumbani
  • kutembea kwenda safari fupi badala ya kutumia gari
  • kupanda ngazi badala ya kutumia lifti
  • kuegesha gari mbali kidogo na ofisi ili kupata nafasi ya kutembea

Kwa wale wenye kazi za kukaa, ni vyema kufuatilia shughuli kwa kutembea kuliko kutumia teknolojia kama kupiga simu kwa mtu uliye naye katika jengo moja, kufuatilia mwenyewe badala ya kutumana na kadhalika.

Mazoezi ni pamoja na kutembea, kukimbia, kuruka kamba, na kuendesha baiskeli. Anza taratibu, fanya mazoezi kwa dakika 20 – 30 na fanya angalau mara 3 – 4 kwa wiki.

Epuka msongo wa mawazo

Kuwa na mawazo mengi kunaweza kukuletea mfadhaiko na magonjwa kama vile kuumwa na kichwa au shinikizo la damu, kukosa usingizi, kukosa hamu ya chakula au unywaji wa pombe kuzidi kipimo. Mambo ya kufanya unapojisikia una uchovu na msongo wa mawazo:

  • fanya mazoezi
  • panga kazi zako za siku
  • jadili matatizo na mtu unayemuamini
  • pumzika vya kutosha

Kutotumia tumbaku

Tumbaku inaweza kutumika kwa kuvuta kama vile sigara/msokoto/kiko, kunusa na kutafuna. Utumiaji wa tumbaku unahusishwa sana na saratani ya mapafu, vidonda vya tumbo, kifua sugu na magonjwa mengine mengi.

Athari za utumiaji tumbaku katika viungo mbalimbali vya mwili

  • nywele kunyonyoka
  • kukunjamana kwa ngozi
  • kutokusikia vizuri
  • saratani ya ngozi, mapafu, na mifupa
  • meno kuoza
  • mapafu kushindwa kufanya kazi vizuri na kupata kifua sugu
  • magonjwa ya moyo na kuziba kwa mishipa ya damu
  • vidonda vya tumbo
  • kubadilika rangi ya vidole
  • kansa ya kizazi na kuharibika kwa mimba au kuzaa watoto walemavu

Punguza unywaji wa pombe

Utumiaji mbaya wa pombe kwa kiasi kikubwa husababisha madhara makubwa kiafya hivyo ni vyema kwa watumiaji wa pombe kunywa pombe kiasi au kuacha kabisa jinsi zinavyoshauri dini mbalimbali.

Madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya pombe

  • huharibu ubongo
  • huharibu ini
  • magonjwa ya moyo na mishipa ya damu
  • ajali za barabarani
  • kuzaa watoto wenye ulemavu
  • kisukari
  • kichocheo cha kuanza kutumia dawa nyingine za kulevya

Faida zitokanazo na kutotumia pombe vibaya

Kutotumia au kunywa tu kwa kiasi kuna faida zifuatazo:

  • hupunguza magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, na kisukari
  • hupunguza ajali za barabarani, utumiaji wa dawa nyingine za kulevya,
  • hupunguza hatari ya watoto kuzaliwa na ulemavu
  • huboresha maisha yako na familia yako kwa ujumla
  • husaidia kupunguza uzani

Mwili wa binadamu haukuumbwa ili kuhifadhi mafuta mengi. Hali ya uzani kupita kiasi na kitambi inahusishwa na madhara mbalimbali ya kiafya.

  • Tags

You can share this post!

DPP apewa siku tatu kuwasilisha ushahidi katika kesi dhidi...

Japan yasitisha mpango wa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe...