• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Serikali yabuni kaunti ndogo mpya

Serikali yabuni kaunti ndogo mpya

Na STEPHEN NJUGUNA

SERIKALI imebuni eneo jipya la utawala katika Kaunti ya Laikipia katika juhudi za kudhibiti visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa eneo hilo.

Hayo yanajiri huku taharuki ikiendelea kushuhudiwa Laikipia Magharibi, siku ambayo Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alizuru eneo hilo kwa mara ya kwanza.

Nyumba saba ziliteketezwa katika shambulio lililotekelezwa na majangili waliokuwa na silaha hatari jana asubuhi. Mbili kati ya nyumba hizo ni za Polisi wa Akiba katika kijiji cha Dam Samaki, eneo la Ol Moran.

Katika mabadiliko mapya yaliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali, tarafa ya Ol Moran ilibuniwa kutoka kwa Kaunti ndogo ya Laikipia Magharibi.

Aidha, tarafa ya Ng’arua ilitengwa kutoka Kaunti Ndogo ya Nyahururu ili kukabuniwa kaunti ndogo mpya ya Kirima.

Makao makuu ya kaunti ndogo ya Kirima sasa itakuwa katika mji wa Ol Moran.

“Katika juhudi za kuimarisha ushirikishi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Kitaifa, Waziri wa Masuala ya Ndani amebuni eneo jipya la utawala,” ikasema ilani kwenye gazeti hilo nambari 9219 ya Septemba na kutiwa saini na Dkt Matiang’i.

Eneo hilo la utawala linafikisha tatu, idadi jumla ya kaunti ndogo katika eneo bunge la Laikipia Magharibi, ambalo ni pana zaidi. Kufuatia hatua hiyo, kaunti ya Laikipia sasa itakuwa na kaunti ndogo sita.

Zile zilizoko Laikipia Magharibi ni; kaunti ndogo ya Nyahururu, kaunti ndogo ya Laikipia Magharibi na sasa kaunti ndogo ya Kirima.

You can share this post!

Waislamu wamlilia DCI akomeshe utekaji

Matiang’i chini ya ulinzi mkali