• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
UMBEA: Je, wewe ni gusa mara moja au mbio ndefu na hufiki ukingoni?

UMBEA: Je, wewe ni gusa mara moja au mbio ndefu na hufiki ukingoni?

Na SIZARINA HAMISI

KULE nchi jirani ya Tanzania kumeibuka gumzo siku za karibuni.

Na maneno yamewalenga vijana ambao wamekuwa wakilalamikiwa hasa na akina dada kwamba wengi wao jogoo halipandi mtungi.

Mazungumzo haya yameniacha na maswali mengi, kwani wanaojadiliana suala hili wengi wao wana umri chini ya miaka 30.

Pamoja nao, wapo akina dada ambao wako kwenye uhusiano na vijana wenzao, ambapo nao wamekuwa mashuhuda kwamba hali sio shwari na hata baadhi yao wanadiriki kusema ni bora kuchangamsha mwili na mwanaume wa umri mkubwa kwani wao humudu yale yanayowashinda vijana wa umri wao.

Kulingana na mazungumzo haya, ukosefu wa nguvu za kiume limekuwa ni tatizo linalowachanganya vijana kwa kiasi kikubwa, hivyo wengi wao wamekuwa wakihangaika kutafuta na kupata suluhisho.

Ingawa inaweza kuwa tatizo kama matatizo mengine, lakini asilimia kubwa ya wanaume huchukulia upungufu wa nguvu za kiume kama ni suala linalofedhehesha na hata kuona aibu kujieleza hadharani.

Majadiliano haya yakajumuisha zile dalili ambazo akina kaka kadha wamekuwa wakikutana nazo wanapokuwa katika shughuli na wawapendao.

Wapo wale ambao walisema wao ni gusa mara moja, kwamba wanapoanza shughuli hatma huwa haizidi dakika moja, hali ambayo huwaacha wenzao wakiwa bado hatihati.

Pamoja nao wapo wanaoeleza jinsi wanavyokosa kabisa hamu ya kuchangamsha mwili, wengine wakiishi bila burudani kwa zaidi ya mwaka.

Katika majadiliano kumekuwa na shuhuda nyingine jinsi ambavyo baadhi yao wanavyokuwa hoi taabani baada ya awamu ya kwanza ya burudani na hata kuhisi kichefuchefu ama kuumwa tumbo.

Halafu kuna wale wa mbio ndefu, kwamba saa nzima anahangaika kupanda mlima na wakati mwingine asifike kule kileleni.

Pamoja na kwamba wengine hudhani kwenda muda mrefu ni ushujaa, mara nyingi mwenendo huu huwa ni dalili za kulegalega nguvu za urijali.

Hivyo kaka iwapo umekuwa ukikutana mara kwa mara na mojawapo ama dalili kadha ya zilizotajwa, huenda ile hali ya upungufu wa nguvu za kiume inakunyemelea na huna budi kuchukua hatua ya kujinasua kabla hali haijakuwa mbaya.

Wanasema mwili haujengwi na matofali bali ni lishe na utaratibu unaojiwekea kuuimarisha siku hadi siku.

Baadhi ya vijana hupendelea zaidi kula raha na starehe na kusahau kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kujiimarisha kiafya. Ni muhimu kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku. Halafu kuna suala la lishe.

Vijana wa mjini wamekuwa na mazoea ya kupendelea zaidi vyakula laini vyenye mafuta mengi kama viazi vya kukaanga, nyama choma mfululizo na kushushia na bia na huku wengine wakitumia sukari nyingi kupita kiasi.

Vitu hivi sio vibaya, vinafaa na vizuri iwapo vitaliwa kwa kiasi, isiwe ndio maisha yako ya kila siku.

Mwanaume unafaa kula vyakula asili ambavyo wale wanaoishi mashambani huvitumia kwa zaidi.

Iwapo kaka unapendelea zaidi kinywaji na unaona mojawapo ya dalili hizo zilizotajwa hapo juu zinakunyemelea, huna budi kuangalia uwezekano wa kupunguza.

Katika yote, jipe amani moyoni, ni vyema kuepukana na vitu, mambo ama watu ambao wanaweza kukuletea msongo wa mawazo, kukukosesha amani na kukuletea sonona.

Jipumzishe vya kutosha na uhakikishe akili yako inakuwa tulivu.Iwapo hali itaendelea kuwa tete hata baada ya kufanya mabadiliko muhimu katika maisha yako, ni vyema uonane na wataalamu ambako utapata ushauri nasaha. Wanasema mwanaume ni mashine.

[email protected]

You can share this post!

Rais wa Estonia ajiunga na Wakenya kwenye mbio katika msitu...

Wakfu wa Jungle Foundation watoa mafunzo ya huduma ya...