• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Kemsa lawamani tena hospitali zikikosa dawa

Kemsa lawamani tena hospitali zikikosa dawa

IRENE MUGO na ELIZABETH OJINA

HOSPITAL katika kaunti kadhaa zimekumbwa na uhaba wa dawa zikiwemo za kukabili maambukizi ya corona.

Katika Kaunti ya Nyeri, gavana Mutahi Kahiga amelaumu Shirika la kusambaza Dawa Kenya (KEMSA) kwa kukosa kusambaza bidhaa muhimu za matibabu kwenye vituo vya afya, ili kudhibiti Covid-19 huku idadi ya wagonjwa ikizidi kuongezeka.

Gavana huyo alisema baadhi ya vituo havina dawa za kutosha huku vingine vikiwa havina kabisa dawa hizo zinazotumiwa kuwatibu wagonjwa wa Covid-19 kutokana na udhaifu wa shirika hilo.

“Inashtua kuwa KEMSA, shirika letu la pekee la kusambaza dawa halina uwezo wa kutusambazia bidhaa muhimu za matibabu licha ya kaunti kuwa na pesa za kununua,” alisema.

Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, hospitali katika wadi, zahanati na vituo vya afya hazijapokea dawa hivyo kuwalazimu wagonjwa kugharimika pakubwa kuzinunua.

Katibu wa Muungano wa Matabibu (KUCO) Craus Okumu, alisema hospitali hazijapokea dawa tangu Aprili.

“Karibu dawa zote muhimu hazipo ikiwemo paracetamol na Amoxicillin. Wagonjwa wetu wanaumia na sisi pia tunaumia ikizingatiwa kuwa tunaandika dawa lakini mgonjwa analazimika kununua kwa sababu hatuna,” alisema Bw Okumu.

Barua

Kupitia barua kwa Katibu wa Kaunti na mkurugenzi wa afya mnamo Agosti 6, maafisa wa muungano wa wafanyakazi wa afya walilalamikia ukosefu wa dawa na vifaa vya matibabu.

Afisa wa Matibabu katika Kaunti Emma Obegi alisema kuwa uhaba huo unatokana na changamoto ya kiufundi kutokana na kuvuka kutoka bajeti ya mwaka mmoja hadi mwingine.

“Pindi tu ununuzi wa dawa utakapoidhinishwa na Msimamizi Mkuu wa Bajeti, ni lazima Hazina ya Kitaifa itatuma pesa ili tuagizie dawa kutoka Kemsa. Kuanzia sasa, tutahakikisha hospitali zinapata vifaa vya matibabu mara tatu kwa mwaka,” alisema Dkt Obegi.

Afisa Mkuu anayesimamia Afya Kisumu, Gregory Ganda, alisema Kaunti hiyo ilikuwa imetenga Sh80 milioni za kununua dawa kutoka Kemsa.

Katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga, Afisa anayesimamia Idara ya Dawa, Lawrence Otieno, alieleza Taifa Leo kwamba hospitali hiyo haijaathiriwa mno kama wenzao katika kaunti hiyo.

“Maafisa wengi wa dawa kutoka hospitali nyinginezo wamekuwa wakija kuomba dawa ambazo hazipo hospitalini kwao. Sisi ni kama kisima cha maji kwenye janga la dawa. Mara kwa mara huenda tukaishiwa na dawa lakini huwa tunahakikisha tuna dawa muhimu zinazohitajika katika kitengo cha dharura na majeruhi, kitengo cha akina mama kujifungulia na upasuaji,” alisema Dkt Otieno

You can share this post!

Kamket huru kwa bondi, azuiwa kukanyaga guu Baringo

CHOCHEO: Zidisha mashamsham, sizubae!