• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
FUNGUKA: ‘Sitoi hata ndururu’

FUNGUKA: ‘Sitoi hata ndururu’

Na PAULINE ONGAJI

TANGU zamani, mzigo wa kukidhi mahitaji ya kifedha ya familia, umekuwa ukielekezewa mwanamume.

Lakini kwa Jason, mhasibu wa kampuni moja jijini Nairobi na ambaye kwa viwango vya kisasa anapata mshahara wa juu, hiyo ni ndoto.

Kaka huyu ambaye ameoa kwa miaka mitano sasa anasema kuwa pesa zake kamwe hazimhusu mkewe.

Kwa kipindi cha miaka kumi ambayo amehudumu katika nafasi hii kazini, kaka amejiundia mali si haba ambayo mkewe hana habari.

Anamiliki fleti ya orofa nne ya nyumba za makazi, ambayo humletea zaidi ya Sh150,000 kila mwezi.

Isitoshe, ana magari matatu ya uchukuzi yanayohudumu jijini Nairobi.

Lakini licha ya mali hiyo yote, ameapa kutonunua chochote nyumbani na mzigo wote wa kifedha anaubeba mkewe ambaye ni mchuuzi.

Licha ya kuwa kazi hii ina mapato, pesa hizi hazipatikani kila siku.

Jason anapoulizwa kwa nini akaamua kuchukua msimamo mkali hivi, jibu lake huwa sahili.

“Mali niliyonayo niliipata kupitia mikopo ambayo ni mimi mwenyewe niliyolipia, kumaanisha hakuna mtu mwingine atakayenufaika na jasho langu. Siwezi ‘nunua hata mboga kwani siku hizi hata wanawake wanapaswa kugawana mzigo wa kifedha. Nikijumuisha mapato yangu kutokana na biashara zangu na mshahara ninaopokea kila mwezi, natia kibindoni zaidi ya Sh250,000, lakini lazima mwanamke ahangaike.

Mwisho wa mwezi lazima alipe kodi ya nyumba, anunue chakula, awalipie watoto karo, awanunulie nguo na pia baada ya hayo yote, anipe haki yangu.

Kwa upande mwingine, katika biashara yake ameniandika kama mmoja wa wanufaishwa, ambapo endapo jambo lolote litamfanyikia, basi mimi ndiye mrithi.

Lakini mimi sijamjumuisha kwenye orodha ya wanufaishwa kazini kwangu. Kwa sasa mke wangu amenunua kipande cha ardhi na tayari ameanza ujenzi wa nyumba yetu tunayomiliki pamoja licha ya kuwa sikuchangia hata senti moja. Nilichukua uamuzi huu baada ya kushuhudia kisa cha mjomba wangu aliyekuwa na tabia ya kumfichulia mkewe kila kitu.

Mwanamume huyo alikuwa amemweka mkewe kama mnufaishwa wa mali yake.

Kama wengi walivyotabiri, bwana huyo alikufa kwa njia za kutatanisha na binti akachukua usukani na kusimamia mali yote huku akitumia utajiri alioachiwa kuburudisha madume barobaro.

Isingelikuwa jitihada za familia ya marehemu kuingilia kati na kuelekea kazini kusitisha malipo ambayo binti alikuwa akitarajia kutokana na kifo cha mumewe, basi watoto hao wangeachwa bila chochote. Nd’o sababu niliamua kujipanga na kuhakikisha kuwa hakuna wakati hata mmoja ambapo mwanamke nisiye na uhusiano wa damu naye, atatumbuizwa na jasho langu”.

You can share this post!

CHOCHEO: Zidisha mashamsham, sizubae!

TAHARIRI: Tuwekeze katika soka ya kina dada