• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Vilio vya Muturi, Waiguru vyazua maswali mengi

Vilio vya Muturi, Waiguru vyazua maswali mengi

Na BENSON MATHEKA

MASWALI yameibuka kuhusu madai ya Spika wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru kwamba wanatishwa na taasisi za uchunguzi za serikali kwa sababu ya misimamo yao ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mnamo Ijumaa, Bw Muturi alisema bila kufichua kwamba amekuwa akitishwa na taasisi za uchunguzi tangu alipotangaza kuwa atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kauli yake ilijiri siku moja baada ya Bi Waiguru kuhojiwa na wapelelezi wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) na kudai kwamba hatua hiyo ilitokana na msimamo wake wa kisiasa.

“Mimi na viongozi wengine wanaounga azima yangu ya kugombea urais tumetishwa kuwa tutashtakiwa,” Bw Muturi alisema akiwa nyumbani kwake mashambani Embu.

Bi Waiguru hajatangaza kumuunga Bw Muturi ambaye kufikia sasa ndiye kiongozi wa pekee kutoka Mlima Kenya aliyetangaza kuwa atagombea urais.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kauli za Bw Muturi na Bi Waiguru zinaibua maswali mengi kuhusu anayetaka kuwazima hasa ikizingatiwa kuwa wanatoka kaunti jirani na wamekuwa washirika wakuu wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Vilio kama hivi vimekuwa vikitolewa na washirika wa Naibu Rais William Ruto ambaye ametofautiana na Rais Kenyatta.

Vinapotolewa na mtu kama Spika wa Bunge la Taifa, ambaye ni mwandani wa miaka mingi wa Rais, lazima maswali kuhusu iwapo ni ya kweli, na ni akina nani wanaomuandama hasa ikizingatiwa kuwa anasimamia moja ya nguzo tatu za serikali, yanaibuka,” asema mdadisi wa siasa George Komotho.

Ingawa Bi Waiguru hakuwataja majina aliodai wanamhangaisha kwa kuashiria kuwa atabadilisha msimamo wake wa kisiasa, alisema ni wale waliofadhili mswada wa kumtimua ofisini 2019.

“Wanajulikana, ni wale ambao walitaka niondolewe ofisini,” alisema.

Gavana huyo aliongeza kuwa atawataja majina wakati mwafaka utakapofika.

Bw Muturi ambaye anasimamia Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) alisema kwamba hana rekodi yoyote ya uhalifu, kwa hivyo haogopi vitisho.

“Inaweza kuwa ni mbinu ya kisiasa ya kulenga kuonyesha kuwa yeye si mradi wa serikali au inaweza kuwa mbinu ya kuvutia uungwaji baada ya kugundua wimbi la siasa mashinani linaelekea upande mwingine. Pia inaweza kuwa ni kweli kwa kuwa mazingira ya siasa hubadilika wakati wa uchaguzi ambao Rais aliye mamlakani anaondoka,” asema mchanganuzi wa siasa Geff Kamwanah.

Anasema huenda kuna watu wanaohisi kuwa Muturi anaharibu mipango yao kwenye uchaguzi mkuu ujao au yeye binafsi atake kujipanga nje ya makwapa ya Rais Kenyatta ambaye anaondoka mamlakani.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Muturi na Bi Waiguru wanataka kujenga himaya yao ya kisiasa nje ya kivuli cha rais na hii inaweza kukasirisha baadhi ya watu wanaotaka siasa za eneo la Mlima Kenya kuchukua mwelekeo fulani,” asema Bw Kamwanah.

Kulingana na Bw Muturi, atagombea urais kwa tiketi ya chama atakachotangaza hivi karibuni. Naye Bi Waiguru alisema kwamba atatangaza mwelekeo wake wa kisiasa baada ya kushauriana na wakazi wa Kirinyaga na eneo pana la Mlima Kenya.

You can share this post!

Kesi ya Jumwa yaahirishwa wakili Ombeta amalize kesi ya...

Kibarua kizito kwa ‘warithi’ 4 wa Joho