• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Wasiwasi KRA ikifunga akaunti za chuo kikuu kwa deni kuu

Wasiwasi KRA ikifunga akaunti za chuo kikuu kwa deni kuu

Na BERNARD MWINZI

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), imefunga akaunti za Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), na kusababisha wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi, wanafunzi na washirika wake wa kibiashara.

Hii ni thibitisho la changamoto za kifedha zinazovikumba vyuo vikuu vya serikali humu nchini.

Duru zilisema kwamba KRA imechukua hatua hiyo baada ya chuo hicho kushindwa kuwasilisha mabilioni ya fedha za ushuru, na ada nyinginezo, kinachokata kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi.

Ripoti ya ukaguzi wa kifedha wa 2020 inaonyesha kuwa KU inadaiwa zaidi ya Sh5.6 bilioni na KRA kama malimbikizi ya fedha inayokata kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi.

Pesa hizo ni kama vile za pesheni, ushuru kwa mishahara na ada za bima ya afya.

Kutowasilishwa kwa pesa hizo kunamaanisha kuwa usimamizi wa KU huzielekeza kwa matumizi mengine.

Hatua hiyo imeweka chuo hicho katika hatari ya kushtakiwa na asasi husika za serikali zilizopaswa kupokezwa fedha hizo.

Afisa wa cheo cha juu katika chuo hicho alithibitisha kufungwa kwa akaunti zake na KRA.

Hata hivyo, aliongeza kuwa usimamizi wa KU unafanya mazungumzo na mamlaka hiyo ili uruhusiwe kulipa sehemu za fedha ambazo KRA inadai kufikia Ijumaa wiki jana.

“Baada ya kulipa sehemu ya deni hilo, akaunti zilifunguliwa tena,” afisa huyo ambaye aliomba jina lake libanwe, akaeleza.

Hata hivyo, Taifa Jumapili haikufanikiwa kuthibitisha madai hayo kwa sababu usimamizi wake ulikataa kunukuliwa na ripota wetu.

Hata hivyo, wahadhiri walisema Ijumaa kuwa walianza kupokea mishahara yao ya Agosti.

Ripoti zilisema kuwa KU haijaweza kufadhili shughuli zake za kila siku kutokana na kupungua kwa mapato.

Imekuwa ikilipa mishahara ya wafanyakazi kwa kutumia pesa za mikopo kutoka kwa benki.

Mwezi huu, chuo hicho kiliamua kuwalipa wafanyakazi wake kwa kutumia hundi, ambazo zilikataliwa na benki mbalimbali.Changamoto za kifedha zinazokumba Chuo Kikuu cha Kenyatta zinaakisi, kwa njia zote, zile zinazokumba vyuo vikuu vya umma nchini.

Katika wiki ambayo KRA ilikuwa ikifunga akaunti za KU, wapelelezi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) walikuwa wakichunguza madai ya ubadhirifu na wizi wa pesa katika Chuo Kikuu cha Moi.

Hiki ni chuo kingine kikuu cha serikali kinachozongwa na changamoto za kifedha.

You can share this post!

Kibarua kizito kwa ‘warithi’ 4 wa Joho

Watoto na vijana waanza kupewa chanjo ya corona