• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MAPISHI: Nyama ya kuku yenye ukavu na utamu wa kipekee

MAPISHI: Nyama ya kuku yenye ukavu na utamu wa kipekee

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 30

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • vipande vya nyama ya kuku iliyooshwa na kukatwakatwa kabla ya kukaushwa maji vizuri na kukatwa mistari ili viungo viingie vizuri
  • kitunguu saumu kilichosagwa kijiko 1
  • paprika kijiko 1
  • chicken masala kijiko 1
  • pilipili manga iliyosagwa kijiko 1
  • ndimu/ limau moja
  • breadcrumbs yaani chembechembe za mkate kiasi
  • yai moja
  • chumvi kiasi
  • mafuta ya kukaangia kuku

Maelekezo

Weka kuku kwenye bakuli utie kitunguu saumu, paprika, chicken masala, pilipili manga, maji ya ndimu au limau na chumvi.

Changanya vizuri kisha weka pembeni kwa muda wa nusu saa au zaidi.

Bandika sufuria mekoni, mimina mafuta yaendelee kushika moto.

Changanya lile yai moja pamoja na chumvi kwenye bakuli.

Chukua kipande kimoja kimoja cha kuku utie kwenye mayai kisha kwenye breadcrumbs na hatimaye kwenye mafuta yaliyochemka.

Hakikisha mafuta hayashiki moto sana na pia kaanga kuku kwa moto mdogomdogo ili kila kipande cha kuku kiive vizuri ndani na kiwe na rangi nzuri.

Kila kipande kikishaiva pande zote toa kwenye mafuta. Chakula chako kiko tayari kuliwa.

Maelezo muhimu

Breadcrumbs unaweza ukazipata kwenye dukakuu.

Hakikisha kipande cha kuku unakichovya kwenye mayai na kukitoa papo hapo bila kupoteza muda kwa sababu ukizubaa, viungo vinaweza vikatoka kwenye kuku.

Hakikisha kila kipande cha kuku unakikausha vizuri sana baada ya kuosha ili mnofu usitoe maji wakati unatia viungo.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Tengeneza maski ya nywele kwa kutumia...

ULIMBWENDE: Njia asili za kutunza ngozi