• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Wilbaro, Chungwa vyazua mabishano

Wilbaro, Chungwa vyazua mabishano

Na JUSTUS OCHIENG

Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga sasa wanalaumiana kuhusu alama na kauli mbiu za vyama vyao wakiwania kuvutia asilimia 70 ya kura za vijana kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Jana, Dkt Ruto alimsuta Bw Odinga kwa kuendelea kushambulia wilbaro, alama ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), na kampeni yake ya hasla ambayo waziri mkuu huyo wa zamani anasema inagawanya Wakenya.

Bw Odinga amepuuza alama ya chama cha Dkt Ruto akisema kwamba vijana wa Kenya hawahitaji wilbaro lakini mipango mizuri ya uchumi ili wapate kazi bora.

Waziri Mkuu huyo wa zamani pia amekashifu kampeni ya hasla ya Dkt Ruto akisema inazua “migawanyiko na vita vya matabaka kati ya masikini na matajiri.”

Jana, Dkt Ruto aliyehudhuria ibada katika kanisa la The Global Cathedral, Langata, Nairobi alisema kwamba ni wazi kuwa kampeni yake ya hasla imesababisha wimbi jipya Kenya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema kwamba kampeni hiyo imevunja mipaka ya kikabila na kimaeneo na kukumbatiwa na Wakenya wengi wa kawaida.

“Uongozi ujao wa Kenya utatoka kwa mahasla. Niko na hakika kwamba siku zijazo, suluhu ya matatizo tuliyo nayo kama taifa itatoka kwa wasiotarajiwa,” alisema Dkt Ruto.

Naibu Rais pia alimtaka Bw Odinga kuelezea Wakenya manufaa ya chungwa, alama ya chama chake cha ODM kabla ya kukosoa alama ya wilbaro ya chama cha UDA.

“Wiki hii kumekuwa na mdahalo kuhusu alama za vyama. Kwa wale ambao wako na shida na alama ya wilbaro, wanaweza pia kutueleza umuhimu wa chungwa,” alisema Dkt Ruto.

Katika mhadhara kupitia video kwa Chuo Kikuu cha Nairobi kuhusu vijana na changamoto za utaifa wiki jana, Bw Odinga alisikitika kwamba vijana waliahidiwa kazi za kidijitali lakini sasa Dkt Ruto anawapatia wilbaro.

“Vijana ambao waliahidiwa kazi za dijitali, ambao waliahidiwa uchumi wa kutegemea elimu, ambao waliahidiwa ukuaji wa uchumi kwa zaidi ya asilimia 10, sasa wanapatiwa wilbaro na kuambiwa eti Kazi ni Kazi,” Bw Odinga alisema.

Aliongeza: “Huu ni ulaghai. Hiyo ni njia ambayo naahidi Wakenya sitafuata.” Jana, Dkt Ruto alihimiza vijana nchini kujitokeza kutumia uwezo wao kwa kuwa wao ni asilimia 70 ya idadi ya Wakenya wote.

“Mtu yeyote asidharau ujana wenu lakini kuweni mfano. Vijana ndio jamii kubwa zaidi nchini Kenya wakiwa ni asilimia 70. Katika hekima yao, nguvu na akili kunapatikana suluhu ya ukosefu wa ajira, biashara tunayotafuta kama nchi,” alisema.

Aliwahimiza vijana wasikubali kudharauliwa na kuwataka wawe mfano kwa kuamua hatima ya nchi yao. “Tunahitaji kuungana kama Wakenya na kumaliza migawanyiko ya kikabila, rangi, dini na kuwa kuwa jamii moja ya Wakenya.”

Hili ndilo ombi langu kuunda nguzo ya urafiki na umoja na ushirikiano ili tuweze kujenga taifa tutakalotoshea wote na ambalo kila mmoja atakuwa na nafasi sawa na jirani yake,” aliongeza Dkt Ruto.

You can share this post!

Mamilioni yatakayotumiwa na serikali kwenye mbio za Kip...

ODM na PAA wazozania umiliki wa afisi mjini Malindi