• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
Wanasiasa wasukuma vijana wachukue vitambulisho

Wanasiasa wasukuma vijana wachukue vitambulisho

Na GEORGE ODIWUOR

WANASIASA katika eneo la Nyanza wamelaumiwa kwa kuwasikuma vijana wachukue vitambulisho kila mara uchaguzi unapokaribia huku idadi ya wanaotuma maombi ikiongezeka na kuchelewesha zaidi mchakato wa kupewa stakabadhi hiyo muhimu.

Shirika la Kitaifa la Usajili wa Watu limesema kuwa linatarajia maombi mengi ya vijana wanaotaka vitambulisho huku kampeni za 2022 tayari zikiwa zimeshika kasi.

Wingi wa maombi ya vitambulisho huwapa makarani presha ilhali shughuli hiyo ikifanyika wakati ambapo uchaguzi upo mbali, stakabadhi hiyo hupatikana haraka bila makosa.

Wiki jana, Kinara wa ODM Raila Odinga akiwa eneobunge la Rangwe, Kaunti ya Homa Bay alidai kuna vijana milioni sita katika ngome yake ya kisiasa ambao wanahitaji kupata vitambulisho.

Aliwataka vijana hao wajisajili kama wapigakura ila hilo litatimia tu iwapo watakuwa na vitambulisho.

Hasa, Bw Odinga aliwaeleza wafuasi wake kuwa hatawania kiti cha urais iwapo hatahakikishiwa kura nyingi kwenye ngome yake.

Mkurugenzi wa Huduma za Usajili Kaunti ya Homa Bay Rosana Bongwe naye alisema makarani wameanza kuwa na kazi nyingi kutokana na maombi mengi ya vitambulisho.

“Wakati ambapo kuna presha nyingi, watu wengi wakihitaji vitambulisho, mchakato huo huchukua muda huku pia stakabadhi hizo zikiwasilishwa zikiwa zimejawa na makosa. Kwa sasa tunapokea maombi 1,000 kutoka afisi zetu nane kila mwezi,” akasema Bi Bongwe.

Afisa huyo alilitoa wito kwa watu 6,000 ambao vitambulisho viko tayari wavichukue katika afisi yao mjini Homa Bay.

Gavana wa Homa Bay Cyprian Awiti pamoja na wanasiasa wa eneo hilo wameeleza hofu yao kuwa iwapo vijana wengi hawatajisajili kama wapigakura, basi nafasi ya Bw Odinga kuingia ikulu itakuwa finyu mno.

You can share this post!

Kituyi akemea Uhuru, amtaja kama dikteta

Kinara wa chama cha UGM, Neto aitaka IEBC isajili vijana...