• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Raila na Mudavadi wamenyania kura za Magharibi

Raila na Mudavadi wamenyania kura za Magharibi

Na SHABAN MAKOKHA

WANASIASA wakuu nchini wameanza kujivumisha miongoni mwa wakazi wa eneo la Magharibi, huku wakilenga kura nyingi za eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2022.

Naibu Rais Dkt William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi ni kati ya wanasiasa ambao wanaonekana kuzidisha kampeni zao eneo hilo, kila mmoja akifika au kutumia washirika wao kujinadi kwa raia.

Wikendi iliyopita, Bw Odinga aliandaa mkutano wa wajumbe wa ODM katika hoteli ya Golf jijini Kakamega huku akionekana kulenga kudumisha uungwaji mkono wake Magharibi ambapo amewika tangu 1997.

Bw Odinga alikutana na wajumbe hao ambao walitoka katika kaunti za Kakamega, Bungoma, Vihiga, Busia na Trans Nzoia. Baadaye alizunguka mjini Kakamega akiwahutubia wafuasi wake huku akisisitiza kuwa Kakamega ni nyumbani.

Kwenye hotuba yake, Bw Odinga alisisitiza kuwa akipata uungwaji mkono wa jamii ya ‘Mulembe’ basi ana uhakika kuwa kile ambacho amekuwa akilenga atakiwahi mwaka wa 2022.

Aidha, waziri huyo mkuu wa zamani aliahidi kufufua kiwanda cha sukari cha Mumias pamoja na kukuza talanta kwenye fani mbalimbali za michezo ambazo zimekolea eneo hilo.

Vilevile, Bw Odinga kwa mara nyingine alikariri kuwa yeye ni mzawa wa kizazi cha mfalme wa Wawanga, Nabongo Mumia na hakuna mtu ambaye anaweza kumzuia kutembelea eneo hilo.

Mnamo Jumapili, Bw Odinga alikuwa eneo la Butere ambapo alihudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu wa Dayosisi ya Butere, kanisa la ACK, Rose Okeno katika Shule ya Wasichana ya Butere.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Bw Mudavadi pamoja na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula huku Askofu Mkuu wa Kianglikana, Jackson Ole Sapit akiwazuia wanasiasa kuhutubu na kupiga siasa.

Maafisa wengi wa polisi walishika doria mjini Kakamega huku wafuasi wa ODM wakishuku kuwa wenzao wa ANC wangezua vurugu na kumzomea Bw Odinga.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, kutumwa kwa polisi wengi mjini Kakamega ni ishara kuwa umaarufu wa Bw Odinga unaendelea kudidimia.

“Huyu si Raila Odinga ambaye tulimjua. Raila hakuhitaji polisi wengi kiasi kile kabla ya kuandaa mkutano mjini Kakamega. Kaunti hii ilikuwa kama makazi yake ya pili na alikuwa akiitembelea jinsi anavyotaka huku akikaribishwa kwa shangwe,” akasema Bw Andati.

Hata hivyo, Seneta Cleophas Malala na mbunge wa Lugari Ayub Savula nao walimkashifu Bw Odinga kwa kudai kuwa atafufua kiwanda cha sukari cha Mumias, wakidai kuwa kutokana na ushirikiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, kiwanda hicho kingekuwa kinafanya kazi sasa.

Bw Mudavadi na Wetang’ula nao wamekuwa wakiendeleza kampeni kali ya kuhakikisha wapigakura wa eneo hilo wanaelekeza kura zao kwenye kapu moja.

You can share this post!

Kinara wa chama cha UGM, Neto aitaka IEBC isajili vijana...

MSIMU WA KUNUNUA BARAKA