• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Natembeya kuwania ugavana Trans Nzoia

Natembeya kuwania ugavana Trans Nzoia

Na GERALD BWISA

MSHIRIKISHI wa ukanda wa Rift Valley George Natembeya sasa ametangaza azma yake ya kuwania ugavana wa Trans Nzoia katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Natembeya alithibitisha uvumi, ambao umeenea kwa miezi kadhaa, kwamba yeye ni miongoni mwa wanaomezea kiti hicho baada ya Gavana Patrick Khaemba kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.

“Ndio Mungu akipenda nitawania. Nina uhakika navutiwa na kiti hicho,” akasema kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini.

Bw Natembeya akaongeza: “Ukifanya kazi mbali na nyumbani na watu nyumbani wakiona kazi yako nzuri, watakuomba urejee nyumbani ili uwafanyie kazi. Kwa hivyo, watu wa nyumbani wakikuita unapaswa kuitikia wito.”

Kwa kuwa yeye ni mtumishi wa umma, Bw Natembeya sasa atahitajika kujiuzulu ifikapo Februari mwaka ujao, kulingana na kanuni zilizotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika siku za hivi karibuni, mshirikishi huyo wa Rift Valley amekuwa akizuru maeneo mbalimbali katika kaunti ya Trans Nzoia ikakagua na kuzindua miradi ya serikali kuu.

Hatua hii imechangia wakosoaji wake kudai anatumia rasilimali na mamlaka ya afisi yake kujitafutia umaarufu kwa ajili ya kuwania ugavana 2022.

Watu kadhaa wametangaza nia ya kuwania kiti hicho ambacho kinatarajia kuvutia kinyang’anyiro kikubwa.

Hata hivyo, tayari wadadisi wa wanabashiri kuwa Bw Natembeya na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa ndio vifua mbele katika kinyang’anyiro hicho.

Miezi kadhaa iliyopita, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alimpigia debe Bw Natembeya, hatua ambayo ilikasirisha wafuasi wa Dkt Wamalwa ambaye mwandani wa karibu wa kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.

 

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

KAULI YA WALLAH: Ni busara kufikiri badala ya kupapia...

Historia bei ya petroli ikigonga Sh134