• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
CHARLES WASONGA: Serikali izuie wizi wa vyakula vya misaada kwa wahanga wa ukame

CHARLES WASONGA: Serikali izuie wizi wa vyakula vya misaada kwa wahanga wa ukame

Na CHARLES WASONGA

BAADA ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa, kuna uwezekano mkubwa kwamba mashirika mbalimbali ya humu nchini na kigeni yataanza kutoa misaada kwa waathirwa wa hali hiyo.

Misaada hiyo ni kama vile ya kifedha, vyakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi kwa Wakenya hao ambao wengi wao wanakabilia na baa la nja na ukosefu wa maji.

Baadhi ya mashirika ya kigeni ambayo yatatoa misaada ni Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO).Kwanza, serikali inafaa kuwa macho wakati kuziba mianya yoyote ya ufisadi katika shughuli nzima ya usambazaji wa misaada ya chakula na mahitaji ya kimsingi kwa waathiriwa.

Kwa mfano, mnamo mwaka wa 2019, machifu watatu katika kaunti ya Baringo walikamatwa kwa kuiba chakula cha msaada ambacho walipaswa kuwasambazia waathiriwa wa njaa katika eneo bunge la Tiaty.

Kukamatwa kwa maafisa kama hawa kwa kushiriki uovu huo kunamaanisha kuwa kuna wengine wengi ambao walitenda makosa kama hayo ila hawakukamatwa.

Ni jambo la aibu kwa serikali kupokea misaada ya kuwasaidia wahanga wa ukame lakini haiwafikii walengwa baada ya kuibiwa na maafisa wake.

Kwa hivyo, serikali kupitia asasi husika chini ya Wizara ya Fedha na Ugatuzi, inafaa kuzima kabisa uwezekano wa maafisa walavu kutumia madhila ya wahanga wa ukame kujitajirisha.

Pili, huku serikali ikijizatiti kuwasaidia waathiriwa wa ukame kwa njia mbalimbali, muhimu ni kwamba isake suluhu la kudumu kwa changamoto hili ambalo hushuhudiwa nchini karibu kila mwaka.Hii ni kwa sababu ukame hua hauji kwa kushtukia.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga, ambayo ni asasi ya Serikali Kuu, kila mara hutoa tahadhari kuhusu ujio wa hali hii, katika maeneo husika.

Kwa hivyo, ni wajibu wa serikali kuweka mikakati ya mapema ya kuwakinga wananchi dhidi ya kuathiriwa na makali ya kiangazi.

Kwa mfano, serikali inafaa kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya uchimbaji mabwawa na visima vya maji katika maeneo ambayo hukumbwa na ukame kila mara (ASAL).

Kwa mfano, mamilioni ya fedha ambazo sasa Mamlaka ya Kudhibiti Ukame (NDMA) imetangaza kuwa inapanga kutumia kuwapelekea maji wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Kenya, zingetumika mapema kufadhili uchimbaji wa visima.V

isima hivi sasa vingekuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji ambao sasa wanahangaika na mifugo wao ambao wengi wamekufa.

Kwa hivyo, maandalizi ya mapema na uadilifu ndio suluhu la kudumu kwa majanga ya kimaumbile kama vile ukame.

You can share this post!

Shughuli kama nyuki JKIA wanariadha wakianza kumiminika kwa...

Gavana Waiguru, Kibicho wazika uhasama