• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Bei: Wakenya waishiwa pumzi

Bei: Wakenya waishiwa pumzi

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI imeshutumiwa na wananchi kwa kuendelea kufanya maisha yao kuwa magumu zaidi kwa ongezeko la kiholela la bei za bidhaa muhimu.

Hatua ya majuzi ni kupandishwa kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta taa, hatua ambayo imewakatiza tamaa ya kuishi Wakenya wengi kwa kushindwa kutimiza mahitaji ya kimsingi ya familia zao.

Wote waliozungumza na Taifa Leo jana walieleza kusononeshwa na maisha kwa kushindwa hata kulisha familia zao, wakati ambapo Kenya imeorodheshwa ya nne barani Afrika kwa idadi kubwa ya mabilionea.

Hali hii inaonyesha kuwa rasilimali za kitaifa zinamilikiwa na kundi dogo la mabwanyenye, huku mamilioni wakikosa hata chakula.

Bw Julius Ochego Barongo, 45, alizungumza na waandishi wetu kwa masikitiko jana kuhusu jinsi maisha yake yalivyovurugwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Baba huyo wa watoto wanne, ambaye hufanya kazi katika hoteli jijini Nairobi, anasema hata mshahara wake ni aibu kuutangaza.

“Nyumbani tunatumia mafuta ya taa kupika, na vile yamepanda sijui itakuwaje. Hadi sasa, sijalipa kodi ya nyumba mtaani Airforce, Eastleigh. Chumba ni Sh4,500. Watoto wananitegemea. Nina deni kubwa la karo. Jinsi maisha yanavyoendelea kupanda ndivyo ninazidi kukopa,” Bw Barongo akasema.

Naye James Shitandi, 29, ambaye pia anahudumu katika mojawapo ya maduka ya urembo mjini Nairobi, anaeleza kuwa kutoka na mshahara wa Sh13,000; anapolipa nauli na kodi hubaki bila chochote mfukoni, na inabidi akope kwa ajili ya matumizi mengine.

Bw Rustus Matia, ambaye ni kibarua wa ujenzi mtaani Zimmerman, Nairobi, alieleza kushangazwa na serikali kutojali maslahi ya mwananchi wa kawaida wakati ambao taifa linazidi kuhangaishwa na Virusi vya Corona.

“Serikali inaendelea kutukandamiza wakati ambapo hata vibarua tunavyotegemea havipatikani kwa urahisi,” Bw Matia akateta.

Ni baba wa watoto sita, wote wakiwa shuleni na wanamtegemea kwa karo, chakula, matibabu, mavazi na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Awali, Bw Matia alikuwa akitegemea gesi ya kupikia nyumbani lakini bei yake ilipoongezwa mwezi Julai aligeukia makaa na mafuta ya taa.

“Tunaishi kwa neema za Mungu tu. Viongozi tuliochagua hawatujali,” akasema.Kilio cha mwananchi huyo si tofauti na cha Perkins Agola, ambaye pia hufanya kazi ya mjengo Zimmerman. Bw Agola ana wasiwasi jinsi atakavyomudu mahitaji ya familia yake kupitia ujira wa Sh600 kwa siku.

“Maisha yanazidi kuwa magumu. Kwa mwezi gharama ya kodi ya nyumba na chakula ni Sh6,500 na mshahara ninaopata hautoshi kamwe,” akasema kibarua huyo ambaye ni baba wa watoto watatu.

Nao wakulima wa mahindi kutoka eneo la North Rift wameonya kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kutachangia kupanda kwa gharama ya uzalishaji na hivyo kuongezeka kwa bei ya unga wa mahindi na ngano.

“Utayarisha wa mashamba ya mahindi na ngano hufanywa kwa trakta ambayo hutumia dizeli. Kuongezwa kwa bei yake kutaongeza gharama ya kilimo,” akaeleza Mathew Koech, mkulima kutoka eneo la Saos, Kaunti ya Nandi.

Jijini Mombasa, Mohammed Abdi hana uhakika kama ataweza kuendelea na biashara yake ya tuktuk kufuatia kuongezeka kwa bei ya petroli. Ingawa Mombasa ndiko watu wanalipa bei ya chini zaidi ya mafuta, anasema dizeli kuuzwa Sh113, kutawalazimu kupandisha nauli.

“Nimefanya biashara hii kwa miaka mitano na ina changamoto nyingi. Wenzetu wa matatu mafuta yanapopanda, huwa wanapandisha nauli. Lakini sisi tukiongeza hata Sh10, abiria hututoroka,” akasema.

Kutokana na biashara kuwa ngumu na mafuta kupanda, sasa anapanga kutafuta nyumba ya bei nafuu ili aweze kuendelea kukidhi mahitaji ya familia yake.Mwenzake, Awadh Muhammad anasema, ‘Mke wangu kwa sasa yuko nyumbani. Pesa ninazopata ni kidogo. Inabidi matumizi mengine nikatishe.

Nilikuwa na mipango yangu lakini kwa sasa haiwezekani.’ Katika Kaunti ya Kisumu, wenye magari ya kibinafsi walikasirishwa na nyongeza ya bei ya petroli wakisema hatua hiyo itawaathiri pakubwa.

“Mapato tunayopata haiwezi kukimu mahitaji ya kimsingi ya familia yangu. Maisha yangu yatakuwa magumu zaidi kufuatia nyongeza ya mafuta ya mafuta,” akasema Charles Otieno, 40.

Taarifa ya Winnie Onyando, Sammy Waweru, Barnabas Bii, Farhiya Hussein, Angeline Ochieng

You can share this post!

Ushuru wa juu, madeni yachangia bei za juu za mafuta

Pwani: Kiangazi chaleta maafa