• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Kuongeza bei ya mafuta kunaongezea umaskini Kenya – Kalonzo

Kuongeza bei ya mafuta kunaongezea umaskini Kenya – Kalonzo

Na WINNIE ONYANDO

VIONGOZI wa kisiasa wakiongozwa na Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka waliishutumu serikali vikali kwa kuongeza bei za mafuta ya taa, petroli na dizeli akiitaja kama mzigo kwa mwananchi wa kawaida.

Akihutubia wanahabari Alhamisi, Bw Musyoka alisema kuongezwa kwa bei ya mafuta, kutafanya nchi kushindwa kukabiliana na umaskini.

“Kuongezeka kwa bei za dizeli, petroli na mafuta ya taa kunaonyesha kuwa bei za bidhaa zingine pia zitapanda. Wakenya wengi tayari wanateseka na serikali inawafanya wateseke hata zaidi,” akasema Bw Musyoka.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli pia alisema kuwa rais anapaswa kubaini wazi kwanini bei ya mafuta imeongezwa.

“Tungependa Rais Kenyatta ajitokeze na kutoa taarifa juu ya ongezeko kwa bei za petrol, dizeli na mafuta ya taa. Anapaswa kuelezea Wakenya kwa nini bei zimepanda licha ya nchi kupambana na corona,” akasema Bw Atwoli.

Mfanyabiashara mashuhuri Jimmy Wanjigi pia aliwataka umma kuchukua hatua kuhusu kuongezeka kwa bei ya mafuta.

Haya yanajiri siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA), kutangaza bei mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa.

You can share this post!

Wakenya Twitter wakerwa na kimya cha Raila bei ya mafuta...

Binti ajitunza kwa kuosha magari na pikipiki mjini, Nairobi