• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Wito wawaniaji urais wenye ‘matumaini makubwa’ wampe mwanamke nafasi ya DP 2022

Wito wawaniaji urais wenye ‘matumaini makubwa’ wampe mwanamke nafasi ya DP 2022

Na LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE kutoka eneo la Mlima Kenya wametoa sauti yao wakitaka wapewe kiti cha Naibu Rais wa nchi wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Wanawake hao wapatao 50 walikongamana katika hoteli moja mjini Thika na kusema ya kwamba wanawake pia wana usemi katika siasa za nchi.

Wakiongozwa na Bi Gladys Chania, waliwarai wawaniaji kiti cha urais wawe mstari wa mbele kumteua mwanamke katika wadhifa wa Naibu Rais hasa kutoka Mlima Kenya.

“Eneo la Mlima Kenya lina idadi kubwa ya wapigakura na kwa hivyo ni vyema mwaniaji yeyote wa urais kufikiria kutoa mgombea mwenza kutoka huku,” alifafanua Bi Chania.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kama wapigakura ili ifikapa wakati wa kupiga kura, wajitokeza kwa wingi.

Wananchi pia walishauriwa wasiwe na uhasama miongoni mwao hasa wakati huu taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu mwaka ujao wa 2022.

“Wananchi wasikubali kugawanywa kwa misingi ya ukabila bali wawe kitu kimoja,” alisema kiongozi huyo.

Alisema ukabila ndicho “kidonda kinachotuathiri sisi kama Wakenya ambapo tunafaa kuzika tofauti zetu katika kaburi la sahau”.

Bi Elizabeth Kairemia mwakilishi wa wanawake Meru, ambaye pia anajulikana kama ‘Mama Ufunguo’ amewarai wanawake wote kutoka Mlima Kenya waungane pamoja.

“Huu ndio wakati wa wanawake kuja pamoja ili kuonyesha umoja wao. Hiyo ndiyo njia pekee ya kupewa heshima kama wanawake,” alisema Bi Kairemia.

Aliwataka wanawake wote kutoka eneo la Meru, Tharaka Nthi, na Mlima Kenya Magharibi, waje pamoja na kuzungumza kwa sauti moja.

Aliwahimiza wanawake popote walipo wawanie viti vya uongozi kutoka udiwani (MCA), ubunge, useneta, hadi ugavana.

“Sisi kama wanawake tuna uwezo wa kupata viti vingi vya uongozi mradi tu tuwe na umoja na uelewano wa pamoja,” alisema kiongozi huyo.

Alisema wataanza kuzuru sehemu tofauti za nchi ili kuwarai wanawake wasikae kando ya uongozi bali wawe mstari wa mbele ili wajitambulishe kwa wananchi.

You can share this post!

Matatu zaendelea na huduma licha ya uvumi wa mgomo

Wakenya Twitter wakerwa na kimya cha Raila bei ya mafuta...