• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Muturi atoa ishara anaelekea kwa Ruto

Muturi atoa ishara anaelekea kwa Ruto

Na WANDERI KAMAU

MIENENDO na semi za kisiasa za Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa katika siku za hivi karibuni, zimeashiria kwamba huenda anajitayarisha kuhamia kambi ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto.

Tangu kutangaza azma ya kuwania urais mnamo Julai, Bw Muturi amekuwa akilalamika kuhusu “kuhangaishwa na watu maarufu serikalini”, kauli sawa na ambazo zimekuwa zikitolewa na waandani wa Dkt Ruto.

Wakati wa hafla ya mazishi ya ndugu wawili wanaodaiwa kuuawa na polisi katika eneo la Kianjokoma, Kaunti ya Embu mnamo Agosti, Bw Muturi alisoma hotuba ya Dkt Ruto.

Ni hali iliyoibua maswali ikizingatiwa kuwa maafisa wakuu serikalini wamekuwa wakikwepa kutangamana na Dkt Ruto kwa namna yoyote ile.

Jumamosi iliyopita, Bw Muturi alizikosoa baadhi ya taasisi za serikali, alizodai zinawahangaisha viongozi kutokana na misimamo yao ya kisiasa.

Akiuhutubia ujumbe uliomtembelea nyumbani kwake katika eneo la Kanyuambora, Embu, Bw Muturi alidai kupewa vitisho na maafisa wa Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Ushuru (KRA) kwa kutangaza azma ya kuwania urais 2022.

“Hatutatishika. Niliwaambia niko tayari kuchunguzwa kwani sina lolote la kuogopa. Mnaweza kuwatisha watu lakini si wote. Vitisho dhidi ya viongozi eti watafunguliwa mashtaka kwa kuniunga mkono vinapaswa kukoma. Nitasimama kidete na viongozi wanaotishwa kwa kuunga mkono azma yangu,” akasema Bw Muturi. Kutokana na kauli hizo, wachanganuzi wa siasa wanasema kuna uwezekano mkubwa Bw Muturi anaelekea katika mrengo wa ‘Tangatanga’, ijapokuwa hajatangaza wazi.

“Wakati kiongozi wa hadhi ya juu serikalini kama Bw Muturi anaanza kudai kuna watu fulani wenye ushawishi wanaomhangaisha, hiyo ni ishara ya wazi anajitayarisha kufanya maamuzi makubwa ambayo huenda yakautikisa ulingo wa siasa nchini,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Anasema nyendo hizo ndizo alizoanza kuonyesha Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) alipokuwa akihudumu kama Kiranja wa Wengi kwenye Seneti. Baadaye, alijiunga na ‘Tangatanga’ alipong’olewa kutoka wadhifa huo. Wadadisi wanasema kauli za Bw Muturi ni pigo kubwa kwa juhudi zinazoendelea za kuliunganisha eneo la Mlima Kenya.

“Hili pia ni pigo kubwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, hasa usemi wake kuhusu mkondo wa kisiasa eneo hilo litakalofuata ifikiapo 2022. Ni hali ambayo pia itaathiri sana usemi wake kuhusu yule atakayemrithi kama kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ngome yake,” akasema Bw Mutai.

You can share this post!

Munyes na Keter waitwa na Seneti kuhusu bei ya mafuta

UGUMU WA MAISHA KUZIDI OKTOBA