• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Suluhu aashiria kugombea kiti cha urais mwaka 2025

Suluhu aashiria kugombea kiti cha urais mwaka 2025

Na THE CITIZEN

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu ameashiria kuwa huenda akawania kiti cha Urais mnamo 2025 huku akikanusha vikali madai kuwa yeye ni kiongozi dikteta.

Kiongozi huyo, mwanamke pekee anayehudumu kama Rais Barani Afrika, alishutumu baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikidai hatasimama kiti cha urais 2025.

“Wanatuchokoza kwa kuchapisha kwenye magazeti kuwa Samia hatawania Urais. Nani aliwaambia?

“Tutahakikisha mwanamke ndiye Rais iwapo tutafanya kazi yetu vizuri na iwapo tutaendelea na umoja wetu,” akasema Rais Suluhu akihutubia kongamano la Umoja wa Kimataifa kusherehekea demokrasia.

Kauli hiyo ilifasiriwa kuwa analenga kupigania kiti hicho kupitia CCM mnamo 2025.

Mwezi uliopita, serikali ilipiga marufuku gazeti la chama tawala cha CCM ambalo lilichapisha habari kuwa Rais Suluhu hatawania Urais mnamo 2025.

Marufuku hiyo ilidumu kwa siku 14 na ilikuwa ya kwanza dhidi ya gazeti hilo kwa jina Uhuru tangu Rais Samia aingie mamlakani.

Pia kiongozi huyo alijitetea akisema hajakuwa akiwakandamiza wapinzani wake tangu achukue usukani kutoka marehemu John ‘Pombe’ Magufuli mnamo Machi mwaka huu.

Mwanzo wa utawala wake, kiongozi huyo aliridhiana na upinzani na hata akawaachilia baadhi ya wafungwa wa kisiasa huku pia akiruhusu baadhi ya vyombo vya habari vilivyopigwa marufuku na Rais Magufuli, viendelee na kazi zao.

Hata hivyo, alibadilika dhidi ya wapinzani wake huku kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe akiwa kati ya viongozi waliokamatwa na amekuwa akizuiliwa kwa tuhuma ya kushiriki ugaidi.

Mbowe alikamatwa mnamo Julai na hali hiyo ikazua madai kuwa Rais Suluhu ameanza kumuiga mtangulizi wake marehemu Magufuli.

Alizuiliwa pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani baada ya kuitisha kikao na wanahabari kuzungumzia mabadiliko ya katiba.

“Tanzania ni nchi ambayo inazingatia demokrasia. Najua kuna changamoto kadhaa ila hii ni kawaida kwa sababu hakuna nchi ambayo haikosi lawama za hapa na pale,” akaongeza.

Chama kingine cha upinzani ACT nacho Jumatano kilisema Tanzania imeanza kuwa nchi ya uongozi wa kidikteta.

“Serikali imesitisha baadhi ya mchakato wa kidemokrasia kwa msingi kuwa inajenga uchumi wa nchi. Hakuna mtu ambaye ana mamlaka ya kukandamiza uhuru wa raia,” alisema.

Hili lilifanyika chini ya utawala wa zamani na linaendelea chini ya uongozi wa sasa,” ACT ikasema kupitia taarifa.

You can share this post!

Wasichana 330,000 walipata mimba 2020 – Ripoti

Mashabiki watiwa nguvuni baada ya vurugu kuzuka wakati wa...