• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
DOUGLAS MUTUA: Rais  Suluhu hasuluhishi, anavuruga

DOUGLAS MUTUA: Rais Suluhu hasuluhishi, anavuruga

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anasuluhisha mambo au anayavuruga kwa raha zake?

Watanzania wanapumua kwa njia huru au bado wamebanwa kama ilivyokuwa enzi ya mtangulizi wa Bi Suluhu, marehemu dikteta John Pombe Magufuli?

Nimesalitika kujiuliza maswali haya hadharani kwa kuwa Rais huyo amedai kuitetea demokrasia ilhali amewafunga jela wapinzani na kuzuia magazeti kuchapishwa.

Hizo si ishara tu za kutokuwapo kwa demokrasia bali ithibati tosha kwamba demokrasia kamwe haipo! Ni sharti tuambizane ukweli hata tukisalitika kwa mama kiasi gani.

Nchi ya Tanzania ni kubwa kumziki mtu yeyote yule, hivyo yote tuliyomtamkia kweupe marehemu Magufuli alipojiona Mungu tutayakariri kwa marudio ili naye Suluhu ayasikie.

Demokrasia, ambayo hakika ni uhuru wa kimsingi wa binadamu, si hisani ambayo wananchi hupewa na viongozi wao wakionyesha tabia njema, la hasha!

Ni stahiki ya mtundu na mtiivu; mnyonge na mwenye maguvu hata ikiwa hawapendi viongozi wake.

Hahitaji kupendwa nao pia ila wana jukumu la kumhakikishia demokrasia. Wao si uhusiano wa kimapenzi bali uhalisia wa maisha yenye mustakabali angavu.

Watanzania wote – wawe wa Chama cha Mapinduzi (CCM); Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo na vinginevyo – wana haki ya kutendewa usawa.

Rais Suluhu alinishtua sana pale serikali yake ilipomkamata na kumzuia kinara wa Chadema, Bw Freeman Mbowe, na viongozi wengine wa Upiunzani mnamo Julai.

Kosa lao? Ati kujiandaa kufanya kikao cha kujadili na kuishinikiza serikali ikubali Tanzania ipate katiba mpya. Walichotwa wote hata kabla ya kikao kuanza!

Bw Mbowe alifululizwa mpaka mahakamani akafunguliwa mashtaka mabaya sana ya kufadhili ugaidi na kula njama.

Ni mtindo wa kileo kwa serikali dhalimu kumsingizia mtu makosa ya ufisadi ili kumpaka tope kimataifa, nchi za nje zimkimbie kama anayenuka, asitue popote pale.

Lakini Tanzania inapaswa kujua Bw Mbowe anasifika kimataifa, hawi wa kiwango hicho hata! Kujaribu kubana usemi wake ni kuupa kipaza-sauti hasa, kumvumisha bila kujua.

Hebu tafakari Raila Odinga akifunguliwa mashtaka ya kubambikiziwa kama hayo uniambie Kenya itakuwaje. Hofu kote-kote, sikwambii wawekezaji wataiambaa kama jini.

Hata baadhi yetu tusioziamini siasa zake za ubinafsi, ujanja na vitendawili bandia tutamwagika barabarani kuishinikiza serikali imwachilie huru mara moja!

Unatambua demokrasia imekomaa si haba pale watu wasiokupenda wanapojitoa mhanga kutetea haki yako ya kusema mambo ambayo masikioni mwao yanaudhi ajabu.

Rais Suluhu anapaswa kukomaa kiasi hicho, apinge vikali jaribio la wahafidhina wa chama chake, CCM, kumshawishi amwogope Bw Mbowe na Upinzani kwa jumla.

Vigogo wa siasa kama vile Bw Mbowe, wakili machachari na jasiri Tundu Lissu na wengineo ni watu wa kuitwa faraghani wampe maoni yao kuhusu utawala kwa jumla.

Hata hivyo, inaonekana wanyonge wa CCM wamefaulu kumkumbusha Rais Suluhu kuwa ni mwanamke, wakamsadikisha kuwasikiza wapinzani ni kuhatarisha urais wake.

Na ameingia woga kiasi kwamba hata magazeti ya CCM yenyewe ameanza kuyafungia kuchapishwa!

Uliza gazeti la Uhuru, linalomilikiwa na CCM, lilipigwa kumbo kiasi gani liliporipoti kuwa huenda Bi Suluhu asiwanie urais ifikapo 2025. Ana hofu kupindukia; anang’ata hapulizi!

Liulize lile la Raia Mwema yaliyolipata lilipomhusisha na CCM gaidi aliyewaua watu wanne jijini Dar es Salaam mwezi jana.

Bi Suluhu anapaswa kuelewa kuwa woga wa aina hii husababisha udikteta, haumpi mtu umaarufu wa kuchaguliwa bali humpa sifa za nduli mnyanyasaji wa kutemwa.

Watanzania nao, ikiwa Bi Suluhu atawanyima haki za msingi ili achaguliwe tena, wanapaswa kumnyima kura kwa fujo na kumsomba mbali pamoja na CCM yake.

[email protected]

You can share this post!

Vita vya simba Kenya na Cameroon wakianza dimba la...

Kanuni mpya kwa walimu wa nyanjani