• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Korti sasa kuamua hatima ya kesi kuhusu CBC

Korti sasa kuamua hatima ya kesi kuhusu CBC

RICHARD MUNGUTI na GEORGE MUNENE

MFUMO wa Elimu na Umilisi (CBC) umepata pigo baada ya mzazi kupitia Chama cha Mawakili nchini (LSK) kwenda kortini akitaka utekelezaji wake usitishwe.

Wakiongozwa na kiongozi wa LSK Nelson Havi, mawakili hao wanaomba mahakama ifutilie mbali CBC na kuagiza kurejelewa kwa mfumo wa zamani wa 8-4-4.

Katika kesi hiyo, Bw Havi anasema mfumo wa CBC haufai na umekuwa mzigo mkubwa kwa wanafunzi na wazazi.

Bw Havi anaomba Jaji Mkuu ateue jopo la majaji wasiopungua watano kushughulikia kesi ya kupinga CBC. Walalamishi wanasema mfumo wa CBC hautawafaidi watoto kamwe kinyume na vile unapigiwa upatu na kuchangamkiwa na Waziri wa Elimu Prof George Magoha pamoja na washikadau wengine.

Bw Havi amesema mfumo wa CBC unawakandamiza wanafunzi anaodai wanabebeshwa mzigo mzito kuliko ufahamu wao na uwezo wa akili zao kuung’amua.

Kupitia wakili wake, Bi Esther Awuor Adero Ang’awa, anaomba mfumo huo usitishwe kutekelezwa mara moja kote nchini hadi kesi aliyowasilisha isikizwe na kuamuliwa.

“Kesi hii inajadili maslahi ya wanafunzi , wazazi na walimu na inateka hisia za wote nchini,” asema Bw Havi katika kesi iliyo na kurasa 162. Wakili huyo ameomba mahakama iratibishe kesi kuwa ya dharura kisha itengewe siku ya hivi karibuni kusikizwa na kuamuliwa.

Bw Havi anaomba agizo litolewe kuzima serikali ikiendelea kutekeleza mfumo huu wa CBC ulioanza kutekelezwa 2019 baada ya kuchukua nafasi ya uliokuwepo wa 8-4-4.

Katika kesi hiyo, amemshtaki Waziri wa Elimu, Taasisi ya Kuunda Mtaala (KICD), Baraza la Mitihani (Knec), Chama cha Walimu (Knut), Bunge la Kitaifa na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i.

Wakili huyo alisema vitendo vya washtakiwa katika utekelezaji wa CBC vinakaidi haki za watoto. “Maisha ya wanafunzi yanakumbwa na hali ya suintofahamu na kizungumkuti kutokana na mfumo huu unaolemea wanafunzi,” akasema Bw Havi.

Pia anaomba mfumo wa CBC usitishwe mara moja kwa vile walimu hawajaandaliwa inavyotakiwa kuutekeleza. Mawakili hao walienda kortini huku Prof Magoha akisisitiza kuwa mfumo wa CBC hautasitishwa.

Akizungumza jana katika hafla ya mahafali katika Chuo Kikuu cha Embu, Prof Magoha aliwataka wanasiasa kukoma kutatiza utekelezaji wa CBC ambao sasa umefika Gredi 5.

“Serikali ya Kenya ikiwa chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta katika maarifa yake, iliamua kuanzisha CBC kwa manufaa ya watoto wetu. Lazima kila mmoja atii mfumo huo wa elimu,” akasema Prof Magoha.

Waziri huyo aliwalaumu wanasiasa kujaribu kuondoa CBC huku akisema kuwa utafiti kamili ulifanywa kuhusu mfumo huo wa elimu.

“Kwa nini mtu ambaye amesoma na ana maarifa anadai kuwa CBC haikupitishwa bungeni? Hati kuhusiana na CBC zilikaa kwa muda wa miezi sita kabla ya kuidhinishwa,” akaongeza Prof Magoha.

Alionya wanasiasa wakome kuingilia CBC akisema wanahatarisha maisha ya watoto zaidi ya 5 milioni.“Watoto si wa vyama vyovyote vya kisiasa na wanapaswa kuachwa ili wasome.

Serikali imechukua elimu kwa uzito na ndio sababu imetoa mafunzo ya CBC kwa zaidi ya walimu 228,000 na hata kuwekeza idadi kubwa ya pesa kwenye mfumo huo wa CBC,” akasema Prof Magoha.

You can share this post!

Bodaboda kutoka Kenya wafurika Uganda kwa mafuta

Magavana wanuia kunyonya raia baada ya 2022