• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Mulee, Twahir wapigwa kalamu na FKF inayotafuta sasa kocha mpya wa Harambee Stars

Mulee, Twahir wapigwa kalamu na FKF inayotafuta sasa kocha mpya wa Harambee Stars

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Jacob “Ghost” Mulee ametimuliwa kutoka “kiti moto” cha timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya maarufu kama Harambee Stars.

Mulee ameondoka Stars ikining’inia pabaya katika kampeni yake ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar anakocheza mshambuliaji matata Michael Olunga aliyetwikwa majuzi majukumu ya nahodha.

Kenya ilitoka 0-0 dhidi ya wageni Uganda Cranes jijini Nairobi mnamo Septemba 2 na kupiga sare ya 1-1 dhidi ya Rwanda jijini Kigali mnamo Septemba 5 katika mechi zake mbili za kwanza za Kundi E.

Mali, ambayo itaalika Kenya mnamo Oktoba 6 na kuzuru Nairobi mnamo Oktoba 12 katika mechi mbili zijazo, inaongoza kundi hilo kwa alama nne. Ilichapa Rwanda 1-0 nchini Morocco mnamo Septemba 1 na kulamizisha sare tasa dhidi ya Uganda jijini Kampala mnamo Septemba 6.

Mulee,53, alikosolewa vikali kwa kumuacha nje nyota wa klabu ya Montreal, Victor Wanyama kwa michuano hiyo miwili ya kwanza. Pia, hakuwaita wachezaji wazoefu kama winga Ayub Timbe, kiungo Johanna Omolo, beki Brian Mandela, kiungo Anthony Akumu na beki Joash Onyango.

Katika taarifa ya kumtimua Mulee iliyotolewa Septemba 15 usiku, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) lilisema kuwa pande hizo zimefikia makubaliano kutengana.Naibu kocha Twahir Muhidin, ambaye kama Mulee aliwahi kuongoza Stars hapo awali, pamoja na kocha wa makipa Haggai Azande, pia walitemwa.

“Manaibu wa kocha Ken Odhiambo na William Muluya watasalia na Stars wakati huu FKF bado inashughulikia kuunda benchi ya kiufundi kabla ya mechi zijazo za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Mali…,” taarifa hiyo kutoka kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno ilisema.

Aliongeza, “Zoezi la kutafuta kocha mpya linaendelea na tutamtangaza hivi karibuni.”Mulee alichukua usukani kutoka kwa Francis Kimanzi mnamo Oktoba 21 mwaka 2020. Katika kipindi chake kifupi usukani, Stars ilibanduliwa kushiriki Kombe la Afrika 2021 baada ya kukabwa 1-1 na kuchapwa 2-1 na wanavisiwa wa Comoros mwezi Novemba 2020 na kutoka 1-1 dhidi ya Misri na kulima Togo 2-1 mwezi Machi 2021 katika mechi za kufuzu.

Orodha ya makocha Harambee Stars imekuwa nao:

Ray Bachelor (1961)

Jack Gibbons (1966)

Elijah Lidonde (1967)

Eckhard Krautzun (1971)

Jonathan Niva (1972)

Ray Wood (1975)

Grzegorz Polakow (1979)

Stephen Yongo (1979)

Marshall Mulwa (1980-1983)

Bernhard Zgoll (1984)

Reinhard Fabisch (1987)

Christopher Makokha (1988)

Mohammed Kheri (1988-1990)

Gerry Saurer (1992)

Mohammed Kheri (1995)

Vojo Gardasevic (1996)

Reinhard Fabisch (1997)

Abdul Majid (1998)

Christian Chukwu (1998)

James Siang’a (1999-2000)

Reinhard Fabisch (2001-2002)

Joe Kadenge (2002)

Jacob “Ghost” Mulee (2003-2004)

Twahir Muhiddin (2004-2005)

Mohammed Kheri (2005)

Bernard Lama (2006)

Tom Olaba (2006)

Jacob “Ghost” Mulee (2007-2008)

Francis Kimanzi (2008-2009)

Antoine Hey (2009)

Twahir Muhiddin (2009-2010)

Jacob “Ghost” Mulee (2010)

Zedekiah Otieno (2010-2011, kaimu kocha)

Francis Kimanzi (2011-2012)

Henri Michel (2012)

James Nandwa (2012-2013, kaimu kocha)

Adel Amrouche (2013-2014)

Bobby Williamson (2014-2016)

Stanley Okumbi (2016-2017)

Paul Put (2017-2018)

Stanley Okumbi (2018)

Sebastien Migne (2018-2019)

Francis Kimanzi (2019-2020)

Jacob “Ghost” Mulee (2020-2021)

?

  • Tags

You can share this post!

Malkia Strikers wang’aria Burundi mtihani mkali dhidi ya...

Aliyelaghai Sh5Milioni ashtakiwa