• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Waliong’ara NSL watuzwa

Waliong’ara NSL watuzwa

NA JOHN ASHIHUNDU

Kocha wa FC Talanta Ken Kenyatta ndiye mshindi wa tuzo ya kocha bora wa Betika Supa Ligi (BNSL) msimu wa 2020/21, baada ya kuiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa ligi hiyo na kuipandisha hadi Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL).

Kenyatta aliwashinda Edward Manoa wa Vihiga Bullets na Benedict Simiyu wa APS Bomet, ambapo makocha hao walipokea Sh500,000, Sh300,000 na Sh200,000 mtawaliwa kwa ushindi wao.

Tuzo ya mchezaji bora ilinyakuliwa Portipher Odhiambo wa Vihiga Bullets kwenye hafla hiyo ya kutoa tuzo iliyofanyika Jumatano katika Serena Hotel, jijini Nairobi.

Kutokana na ushindi huo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 aliweka mfukoni Sh1milioni baada ya kumpiku kiungo mshambuliaji Anthony Gicho wa FC Talanta na Cornelius Juma wa Mwatate United ambao walipata Sh200,000 kila mmoja.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na kocha Edward Manoa. Vile vile nawapongeza wachezaji wenzangu walioniwezesha kuibuka mshindi kutokana na mchango wao,” alisema mwanafunzi huyo wa zamani wa shule ya Menengai High School.

Kwa upande mwingine, kocha Kenyatta alitoa shukrani zake kwa wote waliochangia katika ufanisi wa timu yake ambayo ilimaliza ligi kwa pointi 69, mbele ya Vihiga waliokuwa na 64, huku akiwapongeza viongozi wa timu hiyo wakiongozwa na mwenyekiti Wanjiru Mahihu.

Kabla ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora, Odhiambo ambaye alicheza mechi 25 kati ya 37, alibuka mshindi wa tuzo ya difenda bora na kuweka mfukoni Sh300,000 mbele ya Nichodemus Malika wa FC Talanta na Chris Wilunda wa APS Bomet ambao walipokea Sh200,000 na Sh100,000 mtawaliwa.

Bonface Munyasa wa APS Bomet alitwaa tuzo ya kipa bora, akifuatiwa na Gideon Ogweno of wa Migori Youth huku Wilson Mwangi wa Murang’a Seala akimaliza katika nafasi ya tatu. Walipata Sh400,000, Sh200,000 na Sh150,000 mtawaliwa.

Tuzo ya timu bora ilipewa FC Talanta, wakati kiungo wao Gicho akiibuka kiungo bora na kuondoka na Sh300,000 baada ya kuwashinda Michiri na  Bonface Kweyu wa Vihiga Bullets..

Cornelius Juma aliyeongoza kwa mabao aliibuka mfungaji bora baada ya kumimina wavuni mabao 16 mbele ya Jackson Oketch wa Vihiga na Samuel Ndung’u wa Kenya Police ambao kila mmoja alifunga mabao 15.

  • Tags

You can share this post!

Anaamini talanta ya kuigiza itasaidia wengi miaka ijayo

Malkia Strikers yaungana na Cameroon nusu-fainali ya...