• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Hizi ndizo athari za marufuku kwa wanasiasa madhabahuni

Hizi ndizo athari za marufuku kwa wanasiasa madhabahuni

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya viongozi wa kidini kupiga marufuku siasa kanisani itakuwa pigo kwa wanasiasa wanaotumia ibada kama majukwaa ya kuendeleza kampeni kinyume cha sheria.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba ikiwa marufuku hiyo itatekelezwa kikamilifu, wanasiasa watakosa majukwaa ya kuendeleza kampeni za mapema.

“Wamekuwa wakitumia hafla za makanisa kufanya kampeni za mapema kwa kuwa wanajua kisheria msimu wa kampeni haujaanza. Wanafanya hivyo wakifahamu kuwa polisi hawawezi kuingia makanisani na kutawanya waumini wakati wa ibada,” asema mchanganuzi wa siasa Leonard Ochuka.

Anasema hii imekuwa ikifanikishwa na viongozi wa makanisa ambao wamekuwa wakiwaalika wanasiasa hao kuchanga pesa. “Wakialikwa katika michango wanatumia fursa hiyo kubadilisha hafla za inabada kuwa za kisiasa. Kufaulu kwa marufuku ya viongozi wa makanisa kutatemea utekelezaji wake,” asema Bw Ochuka.

Kanisa Kiangilikana nchini (ACK) lilikuwa la kwanza kupiga marufuku siasa katika kanisa hilo kiongozi wake nchini Jackson Ole Sapit alipowazima vigogo wa kisiasa Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula kuzungumza katika hafla ya kuapishwa Kwa askofu wa dayosisi ya Butere ya kanisa hilo Rose Okeno.

Kulingana na Askofu Sapit, viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia vibaya maeneo ya ibada kwa kuyabadilisha kuwa majukwaa ya siasa.

“Altari makanisani ni za viongozi wa kidini. Wanasiasa wamekaribishwa kushiriki ibada kama washiriki wengine. Wakitaka kuzungumza siasa wafanye hivyo nje ya makanisa,” alisema Askofu Sapit.

Msimamo wake uliungwa na kanisa Katoliki lililosema kuwa wanasiasa wamekuwa wakitumia makanisa kushambulia wapinzani wao. Kulingana na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Nyeri Antony Muheria, wanasiasa wamebadilisha makanisa kuwa majukwaa yao ya kampeni.

“Kwa sababu ya ulafi wao wa kura na umaarufu, wameamua kwamba wanamiliki maeneo ya ibada. Wanataka kuwa na mikutano ya kisiasa makanisani, wanabadilisha maeneo ya ibada kuwa mikutano ya kisiasa kuhutubia watu,” asema Askofu Mkuu Muheria.

Kulingana na Askofu Mkuu Sapit, wanasiasa wameteka makanisa na kuyafanya viwanja vya makabiliano ya kisiasa.

“Kanisa limeacha kutambuliwa kama eneo la ibada na vyombo vya habari vinapeperusha matamshi ambayo wanasiasa wanatoa makanisani na sio mafunzo ya viongozi wa kidini,” alisema Askofu Mkuu Sapit.

Naibu Rais William Ruto na Bw kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa msitari wa mbele kutumia hafla za makanisa kurushiana lawama za kisiasa.

Dkt Ruto amekuwa akichangia makanisa kote nchini huku Bw Odinga akimtaka aeleze anakotoa mamilioni ya pesa anazotoa katika michango hiyo.

Wawili hao, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper na washirika wao wa kisiasa wamekuwa wakitumia ibada kujipigia debe.

Ingawa viongozi wa kidini wanawalaumu kwa kubadilisha makanisa kuwa majukwaa ya kampeni, wadadisi wanalamu viongozi wa makanisa kwa kuwaalika wanasiasa makanisani na kuwa fursa ya kuzungumza na kuchanga pesa.

“Sidhani kuna mwanasiasa anayelazimisha apatiwe nafasi ya kuzungumza kanisani. Ni nafasi wanayopatiwa na wanaitumia kujipigia debe kwa sababu hiyo ndiyo kawaida ya wanasiasa wakisimama mbele ya watu. Hawabagui makanisa, mazishi ambako watu wanaomboleza au mikutano ya hadhara. Mwanasiasa akipatiwa nafasi ya kuhutubu popote pale, kazi yake huwa ni kujipigia debe tu,” asema mdadisi wa siasa James Kisilu.

Anasema kuwa marufuku ya siasa kanisani itatekelezwa kikamilifu iwapo kutakuwa na muafaka kati ya viongozi wote wa makanisa.

“ACK, Kanisa Katoliki, SDA na PCEA yanaweza kutekeleza marufuku hiyo kwa kuwa yako na mfumo wa usimamizi, lakini inaweza kuwa vigumu kwa makanisa la kipentekote ambayo hayana mfumo thabiti wa usimamizi. Mengi yanamilikiwa na watu binafsi na ndio wamekuwa wakialika wanasiasa kwa michango,” asema Kisilu.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa sio mara ya kwanza makanisa kupiga marufuku siasa kanisani na inasubiriwa kuona watakavyotekeleza marufuku ya hivi punde.

Askofu Mkuu Sapit ameonya kuwa atawachukulia hatua viongozi wa kanisa la ACK watakaoruhusu wanasiasa kuzungumza katika makanisa yao.

Vile vile, maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini walikutana wiki hii kujadili suala hilo miongoni mwa mengine yanayohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Kulingana na Ochuka, marufuku ya siasa kanisani inafaa kupanuliwa hadi kwa mazishi.

“Tatizo ni kuwa kuna maeneo ambayo baadhi ya viongozi waanabudiwa hivi kwamba wasipopatiwa nafasi ya kuzungumza ni viongozi wa kidini wanaolaumiwa,’ asema Ochuka.

You can share this post!

Mombasa Olympic Ladies FC yasajili mastaa 10 kupania kurudi...

Magavana waunda vyama vipya kuepuka baridi 2022