• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Tamaa yapelekea hoteli ya kifahari kufungwa

Tamaa yapelekea hoteli ya kifahari kufungwa

Na RICHARD MUNGUTI

WAKURUGENZI watatu wa hoteli iliyo na thamani ya Sh1biliioni walieleza mahakama Ijumaa kwamba tamaa na uhasama baina ya wanahisa zilipelekea hoteli hiyo kufungwa miaka sita iliyopita.

Wakijitetea katika kesi ya wizi wa Sh48.8milioni dhidi yao Lucy Waithera Mwangi,Julius Kariuki Mwangi na John Irungu Githinji walieleza korti “ni tamaa ya wanahisa iliyowasukuma kortini.”

“Sisi hatukuiba pesa hizo miaka 15 iliyopita. Tulitumia pesa hizi kugharamia ujenzi wa mifereji ya kuondoa uchafu, ujenzi wa maduka katika uwanja wa Fig Tree Hotel na ununuzi wa vifaa vya matumizi  kama vile vitanda , magodoro, shuka, vyakula na vyombo vya kupikia na kupakulia wageni vyakula, ”watatu hao walimweleza hakimu mkuu  Francis Andayi.

Bi Lucy Waithera aliyekuwa wa kwanza kujitetea alieleza mahakama  uhusiano wake na mlalamishi katika kesi hiyo aliyepia mkurugenzi wa Fig Tree Stephen Maina Kimang’a ulidorora kitambo.

“Bw Kimang’a amewasilisha kesi chungu nzima dhidi yetu katika idara ya kuamua masuala ya biashara, Mahakama za Kibera na Milimani,” alisema Waithera.Mkurugenzi huyo alieleza korti kesi hizo bado hazijaamuliwa.

Alisema  Bw Kimang’a ambaye yuko na hisa nyingi katika kampuni hiyo 625 amekuwa akiwasukuma wamuongezee mtaji wake wa hisa hadi asili mia 85.Mahakama ilifahamishwa Maina anawasukuma kwa vile baba yake marehemu Benson Kimang’a alikuwa na wake wawili na mke wa kwanza na watoto wake hawakugawiwa chochote  tangu baba yao aage.

“Kimang’a ameshtakiwa na nduguze wakambo wakitaka kupata sehemu yao ya urithi katika mali ya baba yao marehemu.Sasa anatusukuma tumuongeze hisa hadi 85 ndipo apate kitu cha kuwagawia,” Waithera, Kariuki na Irungu walimweleza hakimu.

Waithera anasema pesa wanazoshtakiwa waliiba  zilitumika kuboresha huduma katika hoteli hiyo.Alisema kati ya Sh48.8milioni zilizoidhinishwa na wanahisa 21 wa Fig Tree , Sh22.3milioni zilikabidhiwa  Maina na mahakama alipowasilisha kesi kupitia afisa anayechunguza kesi hiyo inayowakabili.

Waithera alisema pesa walizotumia ni  Sh26milioni na wako na rekodi ya kuonyesha jinsi zilitumika.Mahakama ilielezwa stakabadhi zote za matumizi zilifungiwa katika hoteli wakurugenzi hao walipotimuliwa kwa maagizo ya mahakama.

Waithera alisema “tulitoka tu na nguo tulizokuwa tumevaa. Maina akiandamana na polisi na wahuni walitufurusha kwa hoteli hiyo.”Mahakama iliombwa itembelee hoteli hiyo kujionea jinsi imezorota kufuatia kufungwa kwake 2015.

Bw Andayi atatoa uamuzi Septemba 21, 2021.

  • Tags

You can share this post!

Tamaa yapelekea hoteli ya kifahari kufungwa

Kesi ya ughushi wa vyeti vya elimu dhidi ya mbunge Oscar...