• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Wakenya wamiminika UG kununua mafuta

Wakenya wamiminika UG kununua mafuta

Na WAANDISHI WETU

MAMIA ya madereva katika miji ya Busia na Malaba wamekuwa wakivuka mpaka hadi Uganda kununua mafuta ya magari na pikipiki zao kwa bei nafuu huku malalamishi yakiendelea kufuatia kupanda kwa bei nchini Kenya.

Bei ya petroli nchini Uganda ni Sh110 na dizeli inauzwa kwa Sh102 kwa lita ikilinganishwa na Sh137 na Sh120 mtawalia nchini Kenya.

Wengi wa wanaovuka mpaka kununua mafuta Uganda ni waendeshaji wa pikipiki ambao hawakaguliwi vikali kwenye mpaka.

Wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma pia wamekuwa wakitumia wanabodaboda hao kununua mafuta kwa bei nafuu Uganda.

Mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda Kaunti ya Busia Erick Makokha alisema wanachama 10,000 wataendelea kununua mafuta Uganda na kunyima Kenya ushuru unaohusishwa na kupanda kwa bei za bidhaa hiyo.

“Sisi ni miongoni mwa watu wanaofanya biashara ya mafuta katika nchi. Lakini hatuwezi kuendelea kuteseka katika nchi yetu wakati tunaweza kupata suluhisho katika nchi jirani. Tutakuwa tukinunua mafuta Uganda na kurudi Kenya kwa biashara,” alisema Bw Makokha.

Bw Mohammed Kizito, mhudumu wa kituo cha petroli cha Mukwano mjini Busia, Uganda, alithibitisha kuwa wanauzia Wakenya mafuta kwa wingi.

“Katika siku ya kawaida, tulikuwa tukiuza lita 450 lakini tangu mafuta yapande bei Kenya, tunauza mafuta yote kwa siku,” alisema.

Kupanda kwa bei ya mafuta pia kumefanya magari ya uchukuzi wa umma kuongeza nauli.Safari iliyokuwa ikitozwa Sh100 sasa inagharimu Sh150.

“Abiria wanafikiri kwamba tunawanyanyasa kwa kuwataka walipe pesa zaidi ya walizokuwa wakilipa. Lakini hii ni kwa sababu ya gharama ya mafuta,” akasema Bw Patrick Mombo, dereva wa matatu inayohudumu kwenye barabara ya Busia-Mumias-Kakamega.

Wakati huo huo wazee katika Kaunti ya Tana River wanawataka Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga washinikize wabunge katika kambi zao kubatilisha ongezeko la bei ya mafuta.

Wakizungumza kwenye mkutano mjini Minjila, wazee hao walisema kuwa wawili hao wana uungwaji mkono wa kutosha bungeni. Hivyo basi walikuwa katika nafasi nzuri kuwaamuru wabunge hao kupinga mabadiliko hayo.

“Hawana maana ya kutetea maslahi ya raia wa kawaida katika kampeni ilhali wasipopata nyadhifa hizo watbadilika na kufanya kinyume. Wakati ni sasa kujua ni nani mwenzetu na yupi hasidi,” alisema David Magasani.

Mzee huyo alisema wakati Dkt Ruto na Bw Odinga wanamudu maisha kutokana na pesa za walipa kodi, mkulima wa kawaida hukosa mlo kwa siku kadhaa.

“Huo ni ubinafsi na hakuna ubinadamu kwa wote wawili. Wana uwezo wa kubadilisha hali tuliyopo sasa. Wakishindwa, wasije kuzungumza nasi kuhusu maazimio yao ya mbinu mbadala za kutuinua kiuchumi. Hayatakuwa na maana kwetu,” akasema.

Naye mzee Adams Gurka alitoa wito kwa viongozi hao wawili kuacha kupiga kelele dhidi ya swala hilo la mafuta.

“Watu walichagua Uhuru na Ruto kwa serikali hii wakati bei ya mafuta ilikuwa chini ya shilingi sabini karibu miaka minane iliyopita. Bei zinaweza kubadilika, lakini sio kwa kiwango hiki,” akasema.

Pia, waliwataka Bw Odinga na Dkt Ruto wasitishe ziara zao za kisiasa na waketi na kutatua suala la ongezeko la bei ya mafuta.

Shaban Makokha, Brian Ojamaa na Stephen Oduor

You can share this post!

Arsenal wacharaza Burnley na kupunguzia Arteta presha ya...

Viongozi kukongamana kwa mkutano wa UNGA