• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Wanjigi apata mapokezi mazuri Siaya baada ya kukataliwa Migori

Wanjigi apata mapokezi mazuri Siaya baada ya kukataliwa Migori

Na KENYA NEWS AGENCY

SIKU moja baada ya vijana kuvuruga mkutano wa mfanyabiashara Jimi Wanjigi katika Kaunti ya Migori, mwanasiasa huyo wikendi alipata mapokezi mazuri katika Kaunti ya Siaya ambako ni nyumbani kwa Kinara wa ODM Raila Odinga.

Bw Wanjigi tayari ametangaza kuwa analenga kupigania mchujo wa ODM dhidi ya Bw Odinga, akilenga kupeperusha bendera ya chama hicho 2022.

Mnamo Ijumaa vijana wenye hamaki walivuruga mkutano wa Bw Wanjigi mjini Migori, baadhi wakimlaumu na kudai anatumiwa kuzima ndoto ya Bw Odinga ya kuingia ikulu.

Akihutubu katika miji ya Siaya na Bondo, Bw Wanjigi aliwarejelea vijana waliotibua mkutano wake kama wageni eneo la Migori.

“Walifikiria watatutorosha lakini onge ringo (hakuna kukimbia),” akasema mjini Siaya.

Alijitetea kuwa kama mwanachama wa maisha wa ODM ana kila haki ya kuwania uteuzi wa chama hicho.

Alisisitiza kuwa chama hicho hakitahitaji kuingia kwenye muungano na chama chochote iwapo wanachama wake watafanya kampeni kali ya kukivumisha kote nchini.

“Tufanye kazi pamoja kuhakikisha kuwa ODM inaunda serikali ijayo. Mimi na Raila tuna mbinu ya kuhakikisha hilo linatimia,” akasema Bw Wanjigi.

Alisimulia historia kati yake na Bw Odinga kuanzia mnamo 1991 akisema wamesaidiana kila wakati walikuwa wakiandamwa na tawala mbalimbali.

Wakati huo huo, mshirikishi wa kampeni za Bw Wanjigi Kaunti ya Siaya Mildred Ochieng’ aliokolewa na polisi na kufungiwa ndani ya chumba kimoja katika hoteli ya Gardens, mamia ya vijana walipotishia kumuangushia kipigo wakidai pesa walizoahidiwa wakati wa ziara hiyo.

Vijana hao walikerwa na hatua ya kulipwa Sh500 pekee ilhali walikuwa wameahidiwa Sh5,000.

“Lazima atupatie pesa ambazo tuliahidiwa,” akasema kijana mmoja, akidai Sh500 hata hazikutosha nauli yake hadi Rarieda.

You can share this post!

TAHARIRI: Vijana wasikubali siasa za vurugu

Mishi Mboko ajiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana