• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
ODM haitambui PAA, asema Mbunge

ODM haitambui PAA, asema Mbunge

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) cha Gavana wa Kilifi Amason Kingi kinazidi kupata upinzani mkali mashinani kutoka kwa wanachama wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi.

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire ameapa kupinga kiongozi yeyote atakayeidhinishwa na gavana Kingi kuwania kiti cha ugavana kaunti ya Kilifi.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Bodoi wakati wa uzinduzi wa madarasa manne, Bw Mwambire ambaye ni kinara wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi, alisema ni wakati mzuri wa Gavana Kingi kuwaachia wakazi wa Kilifi kufanya uamuzi wao na kumchagua kiongozi ambaye wanamtaka.

“Tulimpa kazi kama waziri, tukampa nafasi ya kuwa gavana kwa miaka 10, na ni wakati wa kuwaachia wananchi wafanye uamuzi wao na kuchagua mtu anayestahili kuwa gavana. Nitahakikisha mtu huyo hatapita, atakaosa kura yangu na ya wengine wengi ambao ninawawakilisha,” akasema.

Alisema ni wakati wa gavana Kingi kubadilisha msimamo wake.Alikosoa hatua ya Gavana Kingi kuwalazimisha wabunge wa bunge la Kaunti ya Kilifi kuunga mkono chama cha PAA.

Aliwamihiza wabunge hao kuwa imara na kupuzilia mbali vitisho vya gavana huyo.

“Tutawaonyesha kuwa ODM tuko imara zaidi, tunakaribia uchaguzi ujao na tutawaonyesha kuwa tuko sawasawa,” akasema.

Bw Mwambire alikanusha madai kuwa viongozi wa Kilifi walisususia mkutano wa Azimio la Amani jijini Mombasa ulioongozwa na kinara wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Mbunge huyo alisema kuwa mkutano huo ulikuwa wa eneo la Pwani na si wa chama cha ODM.

“Wabunge wa Kilifi walikuwa pale. Hatukutaka kupiga picha ili kuthibitishia watu kuwa viongozi hao wamekuja,” akasema Bw Mwambire.

Alisema magavana watano wa Pwani wanaunga mkono Azimio la Amani ila Gavana wa Kilifi Bw Kingi.

Bw Mwambire alisema chama cha ODM kiko imara na Kilifi inatazamia kufungua ofisi rasmi ya chama hicho hivi karibuni.

“Toka jadi ofisi ya chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi imekuwa ni mtu binafsi. Ilikuwa mwenyekiti wa chama akienda Dubai, ofisi ya ODM iko Dubai. Akiwa Nairobi ofisi ya chama iko Nairobi,” akasema Bw Mwambire.

Alifichua kuwa kinara wa ODM Bw Raila Odinga atahudhuria ufunguzi wa ofisi hiyo na kuwalaki wanachama wapya kirasmi.

“Baba atakuwa hapa kuja kuwapokea rasmi. Tutafanya sherehe kubwa ya kitaifa ya kuwapokea watu wengi ambao wanataka kujiunga kwa chama,” akasema.

Mbunge huyo alieleza kuwa ODM haina mpango wa kufanya muungano na chama cha PAA.

“Hakuna mpango wowote kuwa na majadiliano na chama cha PAA. Katika daftari la kusajili vyama nchini hakuna chama kinaitwa PAA. Tutaongea nao tu watakapokuwa chama rasmi nchini,” akasema.

You can share this post!

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya...

Chebukati apuuzilia mbali madai kuwa ‘deep...