• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
KAMAU: Mizozo UoN inatishia ndoto za vijana wetu

KAMAU: Mizozo UoN inatishia ndoto za vijana wetu

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya ndoto zangu za utotoni ilikuwa kusomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ingawa ndoto za utotoni hubadilika kadri mtu anapokuwa mkubwa, yangu haikubadilika kamwe. Ilibaki kwenye nafsi yangu.

Ulipofika wakati wa kuchagua kozi za kusoma nitakapoingia chuoni, karibu zangu zote zilikuwa katika chuo hicho.

Msukumo wa ndoto zangu ulitokana na sifa nzuri nilizosikia vijijini kuhusu taasisi hiyo, maarufu UoN.

Sifa hizo zilitokana na simulizi za wazee, walimu wangu na maelezo niliyosoma kwenye majarida kadhaa.

Watu wachache waliofaulu kujiunga na vyuo vikuu walikuwa wakialikwa katika shule za msingi kuwapa wanafunzi manufaa ya kujiunga na chuo kikuu.

Walitupa simulizi nyingi za kututia moyo, wakirejelea jinsi chuo cha Nairobi kilichangia uwepo wa watu maarufu kama Prof Ngugi wa Thiong’o, Prof Micere Githae Mugo.

Pia kuna Prof Arthur Obel (aliyeaminika kuvumbua tiba ya virusi vya HIV) na mwandishi Wahome Mutahi (maarufu kama Whispers) kati ya wengine wengi.

Binafsi, nilijipa msimbo wa ‘Whispers Junior’ – kwani nilimuenzi sana Wahome Mutahi na simulizi nilizopewa kumhusu.

Chuo Kikuu cha Nairobi kilikuwa na hadhi kubwa katika jamii kwa mchango wake katika kuendeleza nchi, hasa kupitia sekta ya elimu.

Hata hivyo, inasikitisha kuona taasisi hiyo ikiyumba.

Kwa sasa chuo kinakumbwa na mizozo si haba – hali inayozua wasiwasi kuhusu mustakabali wake.

Mzozo wa kwanza unatokana na tofauti kali ambazo zimezuka kati ya Naibu Chansela, Prof Stephen Kiama, na baadhi ya wasimamizi wakuu kufuatia pendekezo la kubadilisha utaratibu wa kiusimamizi wa UoN.

Mzozo wa pili umeibuka kati ya Prof Kiama na wanafunzi kutokana na hatua ya usimamizi wa chuo kuongeza karo maradufu na kodi ya malazi.

Kwenye malalamishi yao, wanafunzi wanadai hawakushirikishwa hata kidogo wakati maamuzi hayo yakiafikiwa.

Vivyo hivyo, malalamishi kama hayo ndiyo yametolewa na wasimamizi wa idara mbalimbali, ambao hawakuridhishwa na pendekezo la kuunganishwa kwa baadhi ya idara huku zingine zikifutiliwa mbali.

Kimsingi, ni kinaya kwa mizozo kama hii kushuhudiwa katika mojawapo ya taasisi muhimu sana ya elimu nchini.

Taasisi hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kupewa hadhi ya chuo kikuu nchini, baada ya Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa wakoloni.

Kabla ya hapo, Wakenya wengi walioonyesha nia ya kuendeleza walikuwa wakienda katika vyuo vikuu vya nchi jirani, kama Makerere nchini Uganda na kile cha Dar es Salaam nchini Tanzania.

Inavunja moyo kuona mizozo, malumbano na mivutano inayozidi kuchipuka kwani inatishia kuzamisha na kupaka tope taasisi hiyo kubwa zaidi ya elimu ya juu nchini.

Madhara yake yatasambaa mbali kwani yatavunja ndoto za maelfu ya vijana vijijini wanaopania kusomea katika chuo hicho kwa wakati mmoja maishani mwao.

Wito wangu ni kwa usimamizi mkuu wa chuo kusuluhisha mizozo hiyo ili kurejesha hadhi yake tena kama ilivyokuwa awali.

[email protected]

You can share this post!

AKILIMALI: Magurudumu yanamvunia hela, ni kutia bidii tu!

KINYUA BIN KING’ORI: Masharti ya wandani kisiki kwa...