• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
‘Wakenya 103 wamefia Uarabuni tangu 2019’

‘Wakenya 103 wamefia Uarabuni tangu 2019’

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya Wakenya 103 walioenda kufanya kazi Saudi Arabia na mataifa mengine ya Uarabuni tangu 2019 wamefariki, wabunge walielezwa Alhamisi.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Leba wengi wa Wakenya hao ni wale walioajiriwa kama wafanyakazi wa nyumbani katika mataifa ya Saudi Arabia, Qatar, Milki ya falme za Kiarabu (UAE), na Bahrain.

Wao ni miongoni mwa zaidi ya Wakenya l00,000 waliosajiliwa humu nchini na kupelekwa katika mataifa hayo na kampuni mbalimbali ya uajiri, tangu 2019.

Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa na Katibu katika Wizara ya Leba Peter Tum, wengi wa Wakenya hao walifariki kutokana na maradhi kama mshtuko wa moyo, saratani, pumu, Covid-19 miongoni mwa magonjwa mengine.

Hata hivyo, wanachama wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Mwea Josephat Kabinga walipuuzilia mbali sababu hizo na kudai kuwa wengi walifariki baada ya kudhulumiwa na waajiri wao.

“Hii nadharia kuwa vifo hivi husababishwa na mshtuko wa moyo au saratani haina mashiko. Ukweli ni kwamba wengi wao, haswa wale wanaofanya kazi Saudi Arabia hufa kwa kunyanyaswa na waajiri wao,” akasema Bw Kabinga.

Wanachama wa Kamati hiyo waliitaka Wizara ya Leba kuunda ofisi maalum katika mataifa hayo ya Uarabuni ili kufuatilia madhila wanayopitia Wakenya wanaofanya kazi katika mataifa hayo.

“Afisi kama hiyo inafaa kufuatilia hali ya Wakenya haswa wale ambao wameajiriwa kufanya kazi za nyumbani katika mataifa ya Saudi Arabia,” akasema mbunge maalum David Sankok.

“Inasikitisha kuwa huku Wakenya wakiendelea kufariki katika mataifa hayo, Wizara ya Leba haina maelezo kamili kuhusu kiini cha vifo hivyo. Hii ni kwa sababu haina rekodi za watu au kampuni zilizowaajiri Wakenya hao,” akaongeza Mbunge wa Nyatike Tom Odege.

Pendekeza la wabunge hao liliungwa mkono na Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Macharia Kamau aliyehudhuria kikao hicho katika majengo ya bunge.

“Endapo afisi maalum ya wizara ya Leba itawekwa kwa mfano nchini Saudi Arabia balozi wetu nchini humo Peter Ogego atakuwa na kazi rahisi kufuatilia hali za Wakenya wanaofanya kazi katika taifa hilo. Familia za Wakenya hao pia hazitakuwa na wakati mgumu kufuatilia hali za wapendwa wao,” akaeleza.

You can share this post!

Waziri Keter alishwa faini ya Sh500,000 kwa kufeli kufika...

Wapuuza Uhuru