• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Viongozi wamwomboleza wakili Evans Monari

Viongozi wamwomboleza wakili Evans Monari

Na WANGU KANURI

[email protected]

VIONGOZI wanaendelea kutuma salamu za pole kwa familia ya wakili Evans Monari huku wakimtaja marehemu kama mtu shupavu aliyetekeleza kazi yake kwa uadilifu wakati wa uhai wake.

Marehemu Manori alikuwa mmoja wa mawakili ambao walimwakilisha Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akikabiliwa na kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

Viongozi hawa wameandika jumbe zao kwenye kurasa zao za mtandao wa kijamii wa Twitter.

Wakiongozwa na Rais Kenyatta kupitia ujumbe uliochapishwa kutoka ukurasa wa ikulu ya Kenya, viongozi hao wamekumbuka jinsi alivyotia bidii kazini huku akitambulika kama kigogo wa sheria.

“Wakili Monari, mwanasheria ambaye alitambulika kwa ufanisi kazini mwake. Alikuwa mwanasheria ambaye taifa lingetemgemea,” Rais akasema.

Naibu Rais William Ruto, amemtaja wakili Monari kama mwanasheria mwenye maono na ambaye alielewa kwa ukamilifu sheria na katiba.

Naye Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi, ameonyesha kusikitishwa kwake kufuatia kifo chake Manori huku akimtaja kama mwanasheria ambaye alitambulika kwa uzoefu wake katika kazi ya uanasheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Nelson Havi aliposti video ya marehemu Monari akicheza saksofoni. Chini yake akaandika, “Usiku umekuja mwangaza umetoweka. Hakungekuwa na maisha pasi kifo licha ya upweke unaoletwa na kifo.”

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amemwomboleza wakili Manori kama mwanasheria mwadilifu na kiongozi shupavu huku akieleza atakumbuka ucheshi wake na uongozi wake.

Aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale amemtaja marehemu Manori kama mwanasheria aliyeacha nyayo kwenye Mfumo wa Jinai wa Mahakama.

Mwingine aliyemwomboleza ni Seneta Maalum Millicent Omanga.

“Mmoja wa wanasheria shupavu nchini ameondoka. Ninawaombea wanafamilia wake, marafiki na wanasheria wenzake. Paa na malaika mwanasheria Evans Monari,” akaandika Milicent Omanga.

Wakili na Seneta wa Siaya James Orengo amemkumbuka marehemu Monari kama mwanasheria aliyejitolea sana na mwenye bidii.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Ken Monari, wakili huyo amefariki akiwa Nairobi Hospital alipokuwa akipokea matibabu.

Amekuwa akiugua kwa muda.

You can share this post!

Kiboko ahangaisha wakazi wa kijiji cha Nyachaba

Harambee Stars yawasili Morocco kuvaana na Mali...