Habari Mseto

Aagizwa asiseme na mwanamke aliyemtumia picha za uchi

August 20th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Mfanyabiashara Sandeep Ranjikant Desai Alhamisi aliagizwa asizugumze na mwanamke aliyemtumia picha za mtu akiwa uchi.

Hakimu mkuu Abdukadir Lorot alimwamuru Desai “asithubutu kuzugumza na Linda Horpe kwa vile itakuwa anavuruga utekelezaji wa haki.”

Bw Lorot alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Geoffrey Obiri kwamba ” kesi iko mahakamani na mshtakiwa anapasa kuwasiliana na mlalamishi kwa idhini ya korti.:

“Kesi hii imefika mahakamani na mshtakiwa haruhusiwi kamwe kuwasiliana na mlalamishi aliyemshtaki kwa polisi walipofarakana.”

Bw Obiri alisema mshtakiwa anapasa kumweleza afisa anayechunguza kesi dhidi yake iwapo wameafikiana na mlalamishi amwondolee lawama.

“Je, ni mlalamishi aliyepeleka kesi kwa polisi,”Bw Lorot alimwuliza.

“Ndio ndiye aliyenishtaki,” alijibu mshtakiwa.

“Hivyo basi kesi ilitoka mikononi mwa polisi sasa iko kortini.Ikiwa uko na jambo unataka kwa mlalamishi ambaye ni rafiki yako basi itakubidi ueleze korti ikuelekeze utakavyofanya;”Bw Lorot alimshauri mshtakiwa kisha akanzima kuwasiliana na Bi Lorpe.

Hata hivyo Bw Desai alieleza mahakama wanaendelea na mazugumzo na mlalamishi afutilie mbali kesi hiyo.

Bw Desai anakabiliwa na shtaka la kutumia mitandao vibaya kwa kumtumia mlalamishi picha za mtu akiwa uchi akijua “zitamuudhi mno mlalamishi.”

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh30000. Kesi itatajwa baada ya wiki mbili.