Dondoo

Aahidiwa kazi akisaidia kutongoza dada

September 14th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MAVOLONI, YATTA

BUDA mmoja wa hapa aliamua kumwajiri jamaa baada ya kumsaidia kumtongozea dada yake.

Penyenye za mtaani zinasema kuwa buda alikuwa akimmezea mate dada wa jamaa huyo lakini hakuwa amepata nafasi ya kumrushia mistari ya mapenzi.

Jamaa alipata habari kutoka kwa wadaku kwamba buda huyo alikuwa akimtamani dada yake na kwamba binti hakuwa ameingia boksi.

Kulingana na mdokezi, jamaa aliamua kujaribu bahati yake kwa kutafuta kazi kwa bwanyenye huyo ambaye licha ya kuwa na mali hakuwa ameoa.

Siku ya kioja, kaka ya demu huyo alimtembelea buda kwake na kumsihi amwajiri kazi ya shambani.

“Najua unapenda dada yangu sana. Leo ningependa uniajiri kazi hapa kwako. Sina ajira na ninataabika sana nikitafuta kazi,” jamaa alimwambia buda.

Inasemekana badala ya buda kumwajiri jamaa, alimpa kazi ya kumtongoza dada yake ili amkubali.

“Kwanza nitakupa kazi rahisi sana. Kwa hakika nimekuwa nikimtamani dada yako sana lakini hajawahi kunipenda ila mimi ningependa awe mke wangu. Naomba umtongoze aingie boksi ili nimuoe. Akikubali nitakuajiri na kukulipa mshahara mkubwa, tena utakuwa shemeji yangu wa nguvu,” buda alisema.

Inasemekana jamaa alianza kurushia chambo dada yake ili amkubali polo huyo naye apate kazi.

Kwa bahati nzuri demu aliingia boksi baada ya kaka yake kumshawishi amkubali buda huyo.

Mdaku aliarifu kuwa punde tu baada ya buda kufanya harusi na mwanadada, jamaa aliajiriwa kazi ya shambani na kuelezea wenzake alivyomtongoza dada yake ili apate kazi kwa sababu ilikuwa ni vigumu sana kupata kazi kwa buda huyo.