Habari Mseto

Aambia korti mkewe huombea bangi kabla ya kuivuta

November 6th, 2018 1 min read

Na TITUS OMINDE

MUME wa mchungaji mmoja katika mtaa wa Langas mjini Eldoret, alisababsiha kicheko mahakamani alipodai kuwa mkewe huombea bangi yake kabla aanze kuivuta.

Mwanaume huyo ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kupatikana na gramu 500 za bangi yenye thamani ya Sh2,000, aliambia mahakama ya Eldoret kuwa kwake bangi ni dawa na kamwe hataacha kuivuta huku akisifia mke wake ambaye alidai hubariki bangi hiyo kila anapoivuta.

Bw Stephen Maina Mathenge baba wa watoto watano aliambia mahakama kuwa amekuwa akivuta bangi tangu utotoni na anahofia kuwa atakufa akiwacha kuivuta.

“Mheshimiwa kwangu bangi ni kama dawa, hakuna siku nitaacha kuvuta hii sigara kubwa labda nitaacha nikiwa kaburini,” alimwambia Hakimu Mkuu wa Eldoret, Bw Charles Obulutsa.

Hakimu alishindwa kujizuia kucheka kutokana na sarakasi za mshtakiwa ambaye alikiri mashtaka dhidi yake.

Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi wa akili ya mshtakiwa kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret, ilibaini kuwa mshtakiwa ana matatizo ya kiakili ambayo huenda yamechangiwa na uvutaji bangi.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 26 ili kubaini hali ya afya ya mshtakiwa kwa kuwa anapokea matibabu kuhusiana na hali yake kiakili.