Kimataifa

Aanguka na kufariki akipigwa 'selfie' kwenye jabali

June 20th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

KARNATAKA, INDIA

MWANAMUME alifariki alipoanguka kutoka juu ya jabali la maporomoko ya ardhi akijiseti ili apigwe selfie katika Wilaya ya Belagavi, Jimbo la Karnataka.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha kikundi cha vijana katika jabali hilo wakipiga picha, kisha mmoja wao akaenda sehemu ya chini ili apigwe picha ya kipekee.

Lakini mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Ramjan Usman Kagji, 35, alipoteremka wenzake walimwambia apige pozi nyingine ndipo alipoteleza na kuanguka hadi majini.

Ripti za habari zilisema vijana hao walikuwa wamelewa na walionywa dhidi ya kucheza katika eneo hilo linalofahamika kuwa hatari lakini hawakusikia.

Walioshuhudia kisa hicho walinukuliwa kusema wenzake walijutia kushangilia mienendo yake na kumwambia ateremke zaidi.

Mashirika ya habari yalimnukuu afisa wa polisi eneo hilo kusema maji hayo huwa marefu na ilikuwa vigumu kupata mwili wake.

“Si rahisi kujua kweli kama alikuwa mlevi, hilo litajulikana tu baada ya mwili wake kupatikana,” afisa ambaye hakutambuliwa akasema.

Ilisemekana maporomoko hayo ya maji yanayofahamika kama Gokak, huwa kivutio kikubwa cha watalii lakini watu wengi hupoteza maisha hapo kwa ajali na wengine huenda hapo kujitoa uhai.

-Imekusanywa na Valentine Obara