Makala

Aanzisha hazina ya kusaidia wanaougua kifafa

September 21st, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

Baada ya kukumbwa na kifafa, ameamua kusaidia wengine wanaokumbwa na hali sawa na yake. Hii ni hadithi yake Bw Fredrick Kiserem, mwathriwa wa maradhi ya kifafa, na mwanzilishi wa Hazina ya Kiserem Epilepsy Foundation.

Hazina hii inayoendeshwa katika maeneo ya Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, na Lwandeti, Kaunti ya Kakamega , imekuwa hifadhi kwa waathiriwa wa maradhi haya.

“Hasa mradi huu unanuia kuwapa waathiriwa wa maradhi haya, vile vile wengine wenye matatizo ya kiakili, uwezo wa kujitegemea hasa kiuchumi, ambapo tuna chuo cha mafunzo ya ujuzi kama vile ushonaji nguo na useremala, miongoni mwa nyingine,” asema.

Aidha, mradi huu umekuwa ukiangazia mahitaji ya waathiriwa wa kifafa ambapo linawapa sauti ya kuzungumzia wazi masaibu yao, na hivyo kuleta mabadiliko.

“Pia, tumekuwa tukijitahidi kuhamasisha jamii kuhusiana na hali hii hasa ikizingatiwa kwamba waathiriwa wengi hukumbwa na tatizo la kutengwa na unyanyapaa,” aeleeza Bw Kiserem.

Bw Kiserem hakuzaliwa akiwa na hali hii. Masaibu yake yalianza mwaka wa 2011 ambapo alianza kshuhudia mashambulio ya kifafa.

 “Wakati huo nilikuwa nafanya kazi nchini Iraq, na sikujua nini hasa kilichokuwa kikisababisha hali hii. Hata hivyo baada ya kuenda hospitalini, nilifanyiwa uchunguzi, na kutambuliwa kuugua kifafa ambapo  nilianza matibabu mara moja,” aeleza.

Dawa alizokuwa akitumia zilisaidia kudhibiti hali hii ambapo aliendelea kufanya kazi nchini humo kwa miaka miwili zaidi.

Hata hivyo, mwaka wa 2015 hali yake ilizidi kuwa mbaya na akalazimika kurejea nyumbani. “Mambo yaliendelea kuwa mabaya hata zaidi nikiwa nyumbani, ambapo mwaka wa 2016 shambulio la kifafa lilinisababishia majeraha mabaya kiasi cha kunifanya nilazwe hospitalini,” aeleza.

Akiwa hospitalini, gharama ya matibabu ilikuwa zaidi ya Sh 300,000, na anasema ni hapa ndipo alipopata maono ya kuangazia suala hili.

“Nilijiona kubahatika kuwa na pesa za kulipia matibabu hayo, ambapo nilijiuliza je hali ilikuwa vipi kwa wale wasio na uwezo huu? Na hapo nikajituma kuanza kuleta mabadiliko katika nyanja hii,” aeleza.

Japo kwa sasa hali yake imeimarika kabisa kutokana na dawa anazotumia, Bw Kiserem asema kwamba masaibu aliyopitia kutokana na maradhi haya yalikuwa mengi.

“Nakumbuka nikitemwa na mchumba wangu kutokana na hali yangu. Wajua kuna baadhi ya watu wanaohusisha hali hii na ushirikina ambapo kila siku wanawatenga waathiriwa wa maradhi haya.”

Kulingana na Bw Kiserem, umewadia wakati kwa jamii kutambua kwamba hali hii sio mwisho wa maisha. “Kwa kuhakikisha kwamba waathiriwa wanapokea matibabu vilivyo na wanapata usaidizi wa kimaisha, tunaweza ishi maisha ya kawaida,” aeleza.