Dondoo

Aapa kuadhibu mume wake kwa kumchunguza kama ana mpango wa kando

March 18th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

BITOBO, BUNGOMA

Kioja kilizuka katika boma moja la hapa, baada ya mwanadada kuapa kumuadhibu mumewe iwapo ataendelea kumchunguza kisiri.

Kulingana na mdokezi, kipusa alichukua uamuzi huo baada ya kugundua kwamba polo alikuwa akichunguza mienendo yake kisiri kuthibitisha kama alikuwa na mpango wa kando.

Duru zinaarifu kwamba kipusa aligundua tabia ya polo alipoenda kuwaona wazazi wake.

Inadaiwa kwamba kwa muda wote kipusa alikuwa kwao, jamaa alikuwa akipiga kambi karibu huku akichunguza mienendo ya mkewe.

Inasemekana polo alikuwa akiamka asubuhi kwenda kumchunguza na kurejea kwake jioni.

Penyenye zinasema polo alikuwa akimuuliza kila mtu aliyekutana naye kuhusu mienendo ya mkewe.

Habari zinasema baadhi ya wale aliowauliza walienda moja kwa moja na kumweleza mkewe.

“Huyu mtu ana shida gani. Nasikia tangu nije kwetu jamaa yuko tu huku kunichunga. Atanijua siku nitakaporudi kwangu,” mwanadada aliapa.

Kipusa aliporejea kwake, hakumkuta polo. Baada ya dakika chache, jamaa aliwasili.

“Utokako ni wazima?” mkewe alimuuliza polo kwa hasira.  Polo alimuangalia na kushangazwa na swali hilo.

“Nina habari zote. Siku niliyoondoka kwenda kwetu ulinifuata nyuma kisiri. Kwani unafikiria nina wanaume wengine kwetu. Mbona huniamini,” alimshtumu polo.

Inasemekana jamaa aliamua kunyamaza huku mkewe akiendelea kumzomea bila kujali.

Alimkanya mumewe akomeshe hiyo tabia la sivyo atachukua hatua. “Juma lijalo narudi kwetu tena. Jaribu kunifuata tena. Walahi nitawaambia ndugu zangu wakushughulikie. Mimi si mtoto mdogo wa kuchungwa hivyo,” mwanadada aliapa.

“Lazima ujue kwamba wewe ni mali yangu. Lazima nijue kila mahali unakanyaga na wale unaozungumza nao,” polo aliwaka mkewe akatulia.

…WAZO BONZO…