Habari Mseto

Aapa kwa jina la Mola mara 7 akidai polisi walimuumiza sehemu nyeti

February 20th, 2019 3 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa mauaji alisababisha kioja na vicheko mahakamani alipoapa mara saba kwa jina la MUNGU kuthibitisha aliambia mahakama aliumizwa na maafisa wa polisi waliompiga mateke sehemu zake nyeti na kumzamba makofi masikio yakaanza kutoa uzaa.

“Polisi wa kitengo cha Flying Squad walininuzunguka nilipozuiliwa katika kituo cha Muthaiga. Waliniambia nivue nguo na kunipiga mateke sehemu nyeti. Nilipigwa makofi sikio la upande wa kushoto likaziba na kila mara linatoa usaha,” Kachero Peter Ngugi Kamau alimweleza Jaji Jessie Lesiit.

Lakini madai hayo yalipingwa na kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku.

Bw Mutuku alimweleza Kachero Kamau kwamba, “ushahidi wote uliotoa hapa kortini kuhusu kutandikwa mateke sehemu nyeti ni uwongo mtupu. Hii ni hekaya tu kujaribu kukwepa taarifa uliyoandika ukiungama jinsi mliwaua wakili Willy Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri.”

Huku akionekana mwenye wasiwasi, mshtakiwa aliyekuwa na pingu kwenye mkono wa kushoto aliinua mkono wa kulia na kusema, “Nilipofika hapa kortini Septemba 15, 2016 nilieleza mahakama niliumizwa na polisi sehemu zangu nyeti na kwamba naumwa. Niliomba korti iamuru nipelekwe hospitali.”

“Huo ni uwongo, hukuambia korti uliumizwa na polisi uliposhikwa Agosti 8, 2016,” Bw Mutuku akasema.

Wakati huo mshtakiwa alihema huku akibingirisha macho na kuapa. “Haki ya Mungu, Mungu aniadhibu sasa hivi kama sikueleza hii mahakama niliumizwa na polisi nilipokamatwa. Nimeapa kwa Jina la Mungu. Neno la Mungu sio mzaha. Sio uzushi ule tunaozoea. Ukweli ndio huo nilipigwa mateke sehemu nyeti nikaumizwa na sikio la upande wa kushoto.”

Kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku alipopinga madai ya mshtakiwa Februari 20, 2019 katika mahakama ya Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Mshtakiwa aliendelea kusema siku hiyo ya Agosti 8, 2016 alimwonyesha Inspekta Clement Mwangi sehemu zake nyeti anayechunguza kesi ya mauaji ya wakili Willy Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri.

“Je, Inspekta Mwangi alikupeleka hospitali?” Bw Mutuku alimwuliza.

“Hapana, alisema nisubiri wanipeleka katika makazi maalum kwa vile nitakuwa shahidi katika kesi hiyo dhidi ya maafisa wanne wa polisi wa utawala wanaoshtakiwa kwa mauaji ya watatu hao.”

Mshtakiwa alisema pia alimwonyesha Daktari Joseph Wambugu wa Gereza kuu la Naivasha nyeti yake na sikio lake lililokuwa linatoa uzaa.

Bw Wambugu aliamuru Bw Kamau apelekwe hospitali ya Wilaya ya Naivasha alikopewa dawa za kumeza.

Alisema aliagizwa arudi kupimwa tena lakini maafisa wa magereza wakakataa kumrudisha na kumweleza “sio kazi yao.”

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Nelius Mucera Kinyori Bw Kamau alijitetea akisema ushahidi anaodaiwa aliandika alipewa kama umetayarishwa na Insp Mwangi na kutakiwa autie saini.

Bw Kamau alisema ijapokuwa alikuwa ameumia aliamua kunyamaza kwanza atimiziwe ahadi alizopewa na Insp Mwangi.

Akijitetea kuhusu taarifa anayodaiwa aliandika akiwahusisha maafisa wanne wa polisi wa utawala na mauaji ya Kimani , Mwenda na Muiruri mnamo Juni 23 2016 katika eneo la Syokimau , Bw Kamau alitoboa siri kwamba aliahidiwa na polisi atajengewa nyumba , mshahara wa Sh30,000 kila mwezi na mkewe kupewa Sh200,000 kustawisha biashara yake.

“Niliahidiwa kwamba nitakuwa ninapewa Sh30,000 kila mwezi, kufanywa shahidi maalum kama mashahidi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC iliyoko mjini Hague, mke wangu kupewa Sh200,000 kuimarisha biashara yake na kujengewa nyumba,” Bw Kamau alimweleza Jaji Jessie Lesiit alipopinga kutolewa kama ushahidi taarifa ya kurasa 21 aliyoandika.

Bw Kamau alisema alikamatwa kutoka nyumbani kwake mtaani Waithaka na maafisa wa polisiwa Flying Squad baada ya kifo cha wakili Kimani , Mwenda na Muiruri.

Mshtakiwa alisema alipelekwa kituo cha polisi cha Muthaiga ambapo alichapwa kinyama kabla ya afisa wa uchunguzi wa jinai Inspekta Clement Mwangi kuwasili mwendo wa saa mbili usiku.

Mshtakiwa huyo alisema alichapwa baada ya kuwaambia maafisa hao wa polisi wa kitengo cha Flying Squad walimwimbia Sh50,000 alizokuwa ameahidiwa alipowasaidia kukamata wezi waliomnyang’anya Jaji Oscar Angote pesa.

“Maafisa hao wa polisi walinipiga teke sehemu zangu nyeti kisha wakaniumiza sikio hata likaanza kutoa uzaa,” alisema Bw Kamau.

Insp Mwangi alimtoa na kumpeleka makao makuu ya uchunguzi wa jinai (DCI) ambapo alipewa taarifa iliyokuwa imerekodiwa na kutakiwa aitie saini yeye na nduguye John Kamau.

“Nilipoitia saini niliondolewa nikazuiliwa kituo cha polisi cha Thindingua ambapo nilikuwa nalishwa kama mfalme , asububi chai mayai, mandazi, mikate iliyopakwa siagi, nyama choma, ugali na nyama iliyopikwa laini,” Bw Kamau alimweleza Jaji Lesiit.

Baada ya kipindi hicho cha raha mstarehe alihamishwa akapelekwa gereza kuu la Naivasha alikotolewa Septemba 9, 2018 kushtakiwa kwa mauaji ya watatu hao.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Nelius Mucera Kinyori mshtakiwa alikana kabisa aliandika taarifa hiyo na kusema alipewa kama imeandikwa na Insp Mwangi.

Akihojiwa na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ADPP) Nicholas Mutuku, mshtakiwa alikana alieleza mahakama alipigwa na kujeruhiwa na polisi alipofikishwa kortini siku ya kwanza.

Ngugi ameshtakiwa pamoja na Ngugi, Fredrick ole Leliman, Stephen Cheburet, Bi Sylvia Wanjiku na Leonard Maina Mwangi kwa mauaji ya Kimani, Mwenda na Muiruri mnamo Juni 23, 2016.

Kesi itaendelea Machi 6, 2019.