Dondoo

Abebwa juu juu kutumia sheng kanisani

December 2nd, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KAWANGWARE, NAIROBI

HALI ya taharuki ilizuka katika kanisa moja mtaani hapa polo alipotimuliwa kwa kutumia sheng kutoa ushuhuda.

Pasta wa kanisa hilo alimlaumu jamaa kwa kutumia lugha isiyo na adabu wakati wa ibada.

Duru zilituarifu kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa polo huyo kuhudhuria ibada katika kanisa hilo. Ulipofika wakati wa kutoa ushuhuda, alifanikiwa kupata nafasi na akaichangamkia.

“Wasee mimi sina ngori ila kumshukuru sir god. Yeye ndo big man, bazuu na mimi buda siwezi kujichocha ati najiweza. Mashida yakiitana kuitana, sir god wangu hucome kunisave,” polo alisema na kuwashangaza waumini naye pasta akamkatiza.

“Bw Yesu Kristo asifiwe,” pasta alipaza sauti kukatiza kauli ya polo.

“Huyu hapa mwenye lugha kama mkorogo ni baadhi ya mashahidi wa ibilisi wanaotumwa kuvuruga kanisa., Leo atajua hapa ni kanisani si klabu cha mogokaa,” pasta alisema kwa hamaki na kuwaita barobaro waliokuwa wakidumisha usalama katika lango la kanisa.

“Maboys Jo! Kwani nimedo?” jamaa aliwauliza akistaajabu.

Inasemekana mabarobaro hao walimnyanyua huku polo akipigana kwa jino na ukucha lakini juhudi zake hazikufua dafu. Alikuwa mwepesi kama unyoya kwa vijana hao.

“Mabuda, mbona mnanihanda kama makarao? Nimedo?” Alitaka kujua kosa lake.

“Umefukuzwa kutokana na lugha isiyo na heshima na mavazi ya kihuni,” mmoja wao alimwelezea.Kulingana na mdokezi, alikuwa amevalia namna ambayo pasta alidai haingekubalika kanisani.

“Alikuwa na suruali iliyompwaya ungedhani alikuwa na ugonjwa wa kuendesha. Nywele zake za rasta zilikuwa chafu mno. Alivalia fulana iliyombana kuonyesha kifua chake,” alisema mdokezi.

Polo alisalimu amri na kuondoka lakini baadaye pasta alimtafuta na kumshauri baadhi ya waumini walipolalamika.