Habari Mseto

ABIGAEL MWIKALI: Familia ilimuonya uigizaji ungemgeuza hawara, lakini sasa anatamba

February 13th, 2019 2 min read

JOHN KIMWERE,NAIROBI

ANAPENDA kutazama filamu za Soap Opera maana anapania kushiriki uigizaji kufikia viwango vya kimataifa miaka ya usoni.

Hata hivyo ni miongoni mwa waigizaji chipukizi wanaolenga kufanya makuu katika sekta ya filamu nchini.

Mwanzo wa ngoma alikumbana na changamoto kibao ikiwamo familia yake kumpiga marufuku kushiriki uigizaji akidaiwa angeibuka hawara na pia kulipwa mshahara duni.

Mwigizaji huyu anaendelea kujinoa katika uigizaji chini ya kundi liitwalo ‘Goodspel Theatre Production.’

Kundi hilo hutumia mwongozo wa vitabu husika ‘Setbooks’ kuandaa shoo za michezo ya kuigizaji kwenye shule za sekondari katika maeneo tofauti nchini. Japo bado anajihisi hajaiva licha ya kushiriki uigizaji ndani ya miaka minne, anadokeza kuwa amejifunza mengi kimaisha.

Hayo tisa. Kumi huyu siyo mwingine bali ni binti Abigael Mwikali.

Mrembo huyu anasema amefanikiwa kusaidia wenzake wawili kubadilisha mawazo yao walioliwa wamepania kujitoa uhai kutokana na dhiki za maisha. Kipusa huyu aliye meneja wa uzalishaji (production manager), anasema kuwa tasnia ya filamu ina pandashuka nyingi ambapo inahitaji wenye moyo wa kuvumilia.

”Hakika makundi mengi yanayojihusisha na michezo ya kuigiza kupitia miongozo ya vitabu husika hayana uwezo kulipa wasanii wao vizuri,” anasema na kuongeza kuwa hali hiyo hupelekea kujikuta wakikodisha chumba kimoja ambapo hulala zaidi ya wasanii watano wakiwa kwenye ziara za nje ya nyumbani.

Abigael Mwikali. Picha/ John Kimwere

Anasema mtindo huo huchangia wanawake wengi kujikuta njia panda hasa kulazimika kushiriki mapenzi na wenzao ambapo huwa hatari kwao kubeba ujauzito kinyume na matarajio yao.

Hata hivyo anasema kuwa kupitia shughuli hizo amefaulu kutangamana na watu wengi katika sehemu tofauti za taifa hili.

Dada huyu anasema anatamani sana kuibuka mwigizaji wa haiba kubwa duniani. Anataka kufikia kiwango cha staa kama Mercy Johnson aliye kati ya waigizaji mahiri nchini Nigeria.

Veterani huyu amefaulu kushiriki muvi chungu zima tangia ajiunga na tasnia ya filamu mwaka 2004. Aidha ameteuliwa mara 19 kuwania tuzo tofauti kuhusiana na uigizaji na kufaulu kunasa tuzo tano.

Alitwaa tuzo ya ‘Best Actress in Comedy 2013’ shindano Africa Magic Viewers Choice Awards 2013, ‘Popular Choice -Female’ shindano la Nollywood Movies Awards 2014,’ ‘Best Actress in Leading Role’ shindano la Nollywood Movies Awards 2012,’ ‘Best actress in a supporting role’ shindano 5th Africa movie academy awards 2009′, na ‘Best supporting actress’ shindano Best of Nollywood awards 2009.

Pia ameshiriki muvi nyingi tu kama ‘Women in power,’ Into Temptation,’ One-Bullet,’ ‘Oath of a Priest,’ ‘Married to the Enemy,’ ‘Emotional Blunder,’ na Weath Aside,’ kati ya zingine.

Mwikali anasema ugizaji ni kipaji alichokitambua akisoma shule ya upili ya Kyondoni Girls katika Kaunti ya Kitui.

Aidha anadokeza kuwa kando na taaluma hiyo akiwa shuleni pia alikuwa akishiriki kandanda kabla ya kukumbatia masuala ya uigizaji. Msichana huyu alizaliwa mwaka wa 1995 eneo la Katundu Kaunti ya Kitui.