Makala

ABIGAIL KAVISA: Ndoto yangu katika ucheshi ni kufikia upeo wa Trevor Noah

October 28th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

NI binti mchanga na mchangamfu, ambapo ndipo anaanza kuzamia katika tasnia ya ucheshi, ambayo imedhibitiwa kwa muda mrefu na wanaume.

Video zake za ucheshi zimekuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii, ila wengi hawafahamu kwamba safari yake kwenye tasnia hiyo imekuwa ndefu na iliyoanza tangu utotoni mwake.

Je, mwanadada Abbie ni nani? Asili yake ni ipi?

Banati Abigail Kavisa, 20, ni mwanafunzi katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi Nairobi (NIBS) ambako anasomea uanahabari.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Kanzinwa, Kaunti ya Kitui, ambapo baadaye alielekea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Wang’uru, iliyo katika Kaunti ya Kirinyaga.

Anasema hamu ya kutaka kujitosa katika fani ya ucheshi ilianza utotoni mwake.

“Nikiwa katika shule ya msingi, ningewachekesha marafiki wangu kirahisi sana. Wengi walitaka kuwa karibu nami wakati wote. Sikujua nilikuwa na kipaji cha ucheshi,” akasema mwanadada huyo, kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Asema alianza kupalilia kipaji chake, baada ya kugundua kuwa ni talanta ambayo angeitumia baadaye kujipatia riziki.

Jambo lingine lililomsukuma kuingia katika fani hiyo ni kuona mafanikio ya wacheshi wengine, hali iliyomfanya kuamini kuwa kama wao, atafikia mafanikio kama hayo.

Alichukua hatua ya kwanza mnamo 2016, alipojitosa rasmi kwenye fani hiyo.

“Nilianza akaunti yangu ya Youtube, iitwayo Abbiejoy Creations, ambako nilianza kuweka video za ucheshi nilizorekodi. Imekuwa hatua baada ya nyingine. Kufikia sasa, ina zaidi ya washiriki 2,000 lakini idadi hiyo inaendelea kuongezeka,” akasema.

Vile vile, alishiriki kwenye filamu iitwayo ‘Penzi Fiche’ ambayo ilipeperushwa katika runinga ya Kyeni Tv mnamo 2016.

Anasema mipango inaendelea kumwezesha kuanzisha kampuni ya kutayarisha vipindi iitwayo Abbiejoy Productions.

“Lengo langu kuu katika kuanza kampuni ni kunisaidia kuboresha taratibu za kutayarisha video zangu na filamu. Zaidi ya hayo, ninalenga kuwasaidia vijana kutambua vipaji vyao na kuvikuza. Kampuni hiyo itakuwa kama jukwaa la kuwasaidia kujijenga kupitia sanaa ili kutimiza ndoto zao,” akaeleza.

Kwenye safari yake ya ucheshi, baadhi ya watu ambao amekuwa akiwaangalia kama mfano kwake ni wacheshi maarufu kama Trevor Noah, Churchill (Daniel Ndambuki), Victor Naaman, Kayeye the Comedian kati ya wengine.

Anaeleza kuwa kwa sasa, ucheshi ndiyo kazi yake rasmi, kwani huwa inampa kipato.

“Kwa sasa, mimi bado ni mwanafunzi japo huwa nategemea sana sanaa hii kujipa riziki ili kukidhi mahitaji yangu,” asema.

Licha ya mafanikio yake, hajakosa kukumbana na changamoto kadhaa, kama msanii anayechipukia.

Kulingana naye, baadhi ya changamoto zinazomwandama ni ukosefu wa fedha za kutosha kuyatarisha filamu.

“Uandaaji video ama filamu si jambo rahisi hata kidogo. Unahitaji matumizi ya kamera bora ili kuhakikisha kazi inayotoka itawafurahisha mashabiki,” aeleza.

Anasema licha ya changamoto zilizopo katika sekta hiyo, kuna ishara ya hali kuimarika, hasa wakati huu ambapo dunia nzima inakabili janga la virusi vya corona.

Anaeleza ingawa serikali imeweka mikakati kuimarisha tasnia hiyo nchini, juhudi nyingi zinapaswa kuwekwa ili kuiboresha hata zaidi.

Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakimpa msukumo kuendelea kujituma ni familia yake, mashabiki wake na Bi Joy Wangari, ambaye ndiye mtayarishaji wa video zake.

Ushauri wake kwa vijana ni kuendelea kupalilia vipawa vyao, kwani ni kupitia hilo pekee ambapo watatimiza ndoto zao.