Habari Mseto

Abiria aaga kwenye ajali ya barabarani Sachang’wan

May 26th, 2024 1 min read

CHARLES WASONGA NA JIMSON NDUNG’U

MTU mmoja amethibitishwa kufariki katika ajali ya barabara iliyotokea alfajiri Jumapili, Mei 26, 2024 eneo la Jolly Farm, katika barabara kuu ya Nakuru – Eldoret.

Jolly Farm ni kilomita chache kutoka eneo hatari la Sachang’wan, na karibu na kambi ya polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU).

Matatu ya kampuni ya Sifaline Shuttle Ltd iligonga trela kutoka nyuma ilipokuwa ikijaribu kulipita ikiwa kwa mwendo wa kasi.
Ajali hiyo ilifanyika mwendo was aa kumi na moja, asubuhi.

Matatu hiyo inayobeba idadi jumla ya abiria 14 ilikuwa ikielekea Kisumu, kutoka Nairobi, huku trela likielekea Eldoret kutoka Mombasa.

Abiria wengine waliokuwa ndani ya matatu hiyo, walipata majeraha ya kiwango mbalimbali.

“Tulifahamu fika kwamba safari yetu haingekuwa salama dereva na wahudumu wengine wa kampuni hii walipoanza kabla ya gari kuanza safari. Kisha tulipofika Kimende dereva alianza kuyumbayumba huku akipita magari kiholela. Tulimwonya na hakusikia hadi sasa amesababisha ajali hii mbaya,” akasema Mark Oloo, mmoja wa abiria aliyepata majeraha kichwani na mkononi.

Afisa wa trafiki kutoka Nakuru aliyeomba tubane majina yake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na wanahabari, alithibitisha abiria wa kike ndiye alifariki.

“Wanaoguza majeraha mabaya ni watu watano,” afisa huyo akasema.

Dereva wa matatu anasemekana kuwa anauguza majeraha.

Masura hao wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo.

Barabara ya Nakuru – Eldoret, imekuwa ikishuhudia visa vya ajali za mara kwa mara.

Visa vya ajali nchini vinaendelea kuongezeka, mwaka huu, 2024 idadi ikionekana kuwa juu zaidi ikilinganishwa na 2023 kipindi kama hiki (Januari hadi Mei).