Habari

Abiria atolewa kwa ndege baada ya kuiombea ipate ajali

March 11th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME mmoja alitolewa kutoka ndege moja iliyokuwa ikisafiri kwenda Dubai, wakati alipoanza kufanya maombi na kumtaka ‘mungu wake’ kusababisha ajali ya ndege hiyo, kabla ya kupaa kutoka Pakistan.

Abiria huyo ambaye alitambuliwa kwa jina Khalil pekee anasemekana kuwa alianza kuomba mkasa wa mauti utokee punde tu alipoketi ndani ya ndege hiyo, katika uwanja wa kimataifa wa wa ndege wa Islamabad.

Maombi yake yaliwafanya abiria kuhofia na kuanza kuingiwa na wasiwasi, hasa wasafiri na wahudumu wa ndege waliokuwapo.

Khalil alifaa kusafiri kuelekea Australia kupitia Dubai na alikuwa tu ndipo amepanda ndege hiyo jijini Islamabad.

Rubani anasemekana kuwa alitahadharisha idara ya ulinzi katika uwanja huo kufuatia maombi ya kushangaza ya msafiri huyo. Maafisa wa usalama walifika na wakamwondoa kutoka ndani ya ndege.

Hata hivyo, jina lake kamili halikutambuliwa, wala kampuni ya ndege ambayo alikuwa akitumia kusafiri.

Mnamo Novemba 2018, msafiri mwingine aliyekuwa amekasirika alichoma mizigo yake wakati safari yake ilifutiliwa katika uwanja huo wa ndege.

Mwanamume huyo alisemekana kughadhabishwa na hali kuwa ndege aliyopaswa kusafiria ya kampuni ya Pakistan International Airlines (PIA) ilikatazwa kupaa kutokana na hali mbaya ya anga iliyokuwapo.

Msafiri huyo alirekodiwa video akiteketeza mizigo yake, nguo na vitu vingine katika uwanja huo wa Islamabad kabla ya maafisa wa usalama kumzuia.