Habari Mseto

Abiria kunyunyiziwa dawa kabla ya kuabiri feri

April 7th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

MAELFU ya abiria wanaotumia kivuko cha Likoni katika Kaunti ya Mombasa, watakuwa wakinyunyiziwa dawa ya kuua viini kwanza kabla ya kuabiri feri.

Kwenye mpango huo, wakazi hao watalazimika kupita kwenye kibanda ambapo watanyunyiziwa dawa.

Kibanda hicho kimejengwa katika kituo cha kuabiri feri ili kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

Hii ni kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti na mwanasiasa Suleiman Shabhal, shirika la Kenya Red Cross, Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM) na mashirika mengine katika juhudi za kupiga vita maradhi ya COVID-19.

Akizungumza katika kivuko hicho, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, alisema kemikali ambazo zitatumika hazitadhuru afya ya wananchi, kwa kuwa tayari zimepimwa na maafisa wa afya wa kaunti.

“Tutasambaza vifaa vya kutosha vya kujikinga na kemikali. Watu kutoka pande zote za feri watalazimika kunyunyiziwa dawa kabla ya kuabiri feri, ” akasema Bw Joho na kuongeza kuwa pia watapimwa joto.

“Tulivijaribu vifaa kadhaa vya kupima joto siku ya Jumapili. Hata hivyo, tuna wasiwasi sana kuwa hali ya joto ya watu wengine ilikuwa zaidi ya nyuzi 40. Vipimo vya lazima vya joto vitafanyika ili kuhakikisha idadi kubwa ya watu wako salama,” akasema gavana huyo.

Bw Joho aliongeza kuwa vibanda zaidi vitawekwa katika maeneo yenye watu wengi kama vile soko la Kongowea.

“Lazima tutumie kila njia inayowezekana kupiga vita maradhi ya COVID-19,” akasema Bw Joho.

Dkt Josiah Odalo ambaye ni profesa katika Kemia katika chuo cha TUM, aliwahakikishia wakazi kuwa kemikali inayotumiwa ni salama na inaafikiana na viwango vya ubora vinavyotakiwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Prof Odalo alisema kemikali hiyo itasaidia kupambana na virusi, hivyo kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

“Tumeiandaa kwa kutumia rasilimali za kawaida kutoka maabara yetu, ambayo ubora wake umechunguzwa,” akasema Prof Odalo.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, alisema mradi huo utahakikisha usalama wa maelfu ya wakazi kutoka eneo hilo unapewa kipaumbele katika kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.