Habari

Abiy ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kuzima mvutano baina ya Ethiopia na Eritrea

October 11th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amempongeza Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwaka 2019 ya Amani ya Nobel.

Katika pongezi yake, Rais Kenyatta amesema Waziri Mkuu Ahmed anastahili kutambuliwa kimataifa akisema kwamba kiongozi huyo wa Ethiopia ni wa kipekee katika kufuatilia amani, upatanishi na uthabiti nchini Ethiopia, eneo la upembe wa Afrika na bara nzima kwa jumla.

“Ninafurahia ndugu yangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed na watu wa Jamhuri ya Demokrasia ya Muungano wa Ethiopia kwa kutunukiwa tuzo ya mwaka wa 2019 ya Amani ya Nobel. Waziri Mkuu Ahmed astahili kutambuliwa kikamilifu. Amejitokeza wazi kuwa mtetezi shupavu wa amani, uthabiti na ustawi nchini mwake, katika kanda yetu na bara la Afrika,” amesema Rais Kenyatta.

Abiy alitambuliwa kwa juhudi zake za kumaliza mzozo wa miaka 20 kati ya Ethiopia na Eritrea.

“Kamati ya Nobeli la Norway imeamua kumtuza waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali tuzo la amani la mwaka huu,” imesema taarifa kutoka kwa kamati hiyo.

Abiy atakabidhiwa tuzo hilo linaloandamana na zawadi ya Sh93 milioni jijini Oslo, Norway, Desemba 10, 2019.

Juhudi

Akimtangaza mshindi, mwenyekiti wa kamati hiyo, Berit Reiss-Andersen, amesema Abiy anatambuliwa kwa juhudi za kudumisha amani katika upembe wa Afrika.

Ethiopia na Eritrea zilikuwa zikipigania mpaka kati ya 1998 na 2000.

Uhusiano kati ya nchi hizo ulikuwa baridi hadi 2018 Abiy alipoingia mamlakani.

Abiy aliwashinda wengine watatu waliokuwa wameteuliwa akiwemo mwenzake wa New Zealand Jacinda Arden na Raoni Metuktire wa Brazil. Mwingine alikuwa mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg.

Amejiunga na viongozi wengine wa Afrika walioshinda tuzo hilo wakiwemo marehemu Wangari Maathai, Nelson Mandela, Kofi Annan, Wole Soyinka, Ellen Johnson Sirleaf na Albert Luthuli.