Michezo

ABUSO: Dunia iwasaidie wachezaji wa Eritrea

October 7th, 2019 2 min read

Na VICTOR ABUSO

FAINALI ya kuvutia kati ya Kenya na Tanzania ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Jinja nchini Uganda kuwania taji la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20.

Haya ni mashindano yaliyoleta msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka katika ukanda huu na kutoa matumaini kuwa, soka ya Afrika Mashariki na Kati iko mikononi mwa vijana.

Hata hivyo, kuelekea hatua ya nusu fainali, kulitokea mkasa wa kupotea kwa wachezaji watano wa timu ya Eritrea; walitoweka kutoka hotelini na kuzua wasiwasi kuhusu waliko.

Hii si mara ya kwanza kwa kisa kama hiki kutokea hasa kwa wanamichezao wa Eritrea na nchi jirani ya Ethiopia ambao hutumia nafasi hiyo kuomba hifadhi ya kisiasa.

Mwaka 2012, wachezaji wengine 18 walisalia nchini Uganda wakati wa mashindano mengine kama haya, na hali hiyo ikajirudia mwaka 2015, wakati wachezaji 10 waliokuwa wamekwenda nchini Botswana, walipokataa kurejea nyumbani.

Nchini Kenya mwaka 2012, wachezaji 12 wa Eritrea pia walitoweka jijini Nairobi wakati wa mashindano kama haya.

Hatua hii iliwakera viongozi wa CECAFA ambao waliamua kuifungia Eritrea na baadaye kuamua kuirudusha katika mashindano haya mwezi Mei mwaka huu.

Lakini je, wachezaji hawa wanaweza kutoweka vipi, bila ya kufahamika waliko? Hii inamaanisha kuwa wachezaji hawako salama wanapokuwa hotelini. Je ni kwa nini iwe Eritrea na mara nyingine Ethiopia?

Nianze kwa kulijibu swali la tatu kwa nini Eritrea? Hii ni nchi ambayo inapitia changamoto kubwa za kisiasa kwa sababu raia wake wanaishi katika mazingira magumu, hawawezi kusema chochote kinyume na kile ambacho kimepangwa na serikali, kwa kifupi, hakuna upinzani.

Pamoja na hilo, vijana wengi wameamua kujihusisha na mchezo wa soka, wakiwa na matumaini kuwa, siku moja, wataondoka nchini humo na hiyo itakuwa fursa ya wao kuondoka katika nchi yao, kwa sababu ya ugumu wa maisha.

Unapoowangalia wachezaji wa Eritrea, hakika, wana vipaji sana, wana uwezo wa kushinda mechi muhimu.

Hili limeonekana katika michuano ya vijana iliyomalizika huko nchini Uganda. Nakumbuka walifungwa na Kenya bao 1-0 katika hatua ya nusu fainali, na kwa bahati mbaya sana, bao hilo walijifunga wenyewe. Wakati huo wachezaji watano tegemeo, akiwemo kipa walikuwa wameotoweka. Hapo swali ni je, wangekuwepo? Huenda hali ingekuwa vigumu sana kwa vijana wa Kenya.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International, wanaishutumu serikali ya jijini Asmara kwa kuchangia pakubwa kutoweka kwa wachezaji hawa, kwa sababu wanalazimisha vijana kuingia kwenye jeshi, hata ikiwa hawataki.

Naona kuwa njia pekee ya kutatua suala hili ni kwa mazungumzo ili mwafaka upatikane, na wachezaji wa Eritrea wahakikishiwe usalama wao ndani na nje ya nchi ili kupambana na hali hii.

Mwisho, serikali nchini Eritrea ina jukumu la kuacha kuwalazimisha vijana kujiunga katika katika jeshi la nchi hiyo, suala ambalo linaonekana kuwa limeendelea kuwatesa na kutamani kuhama nchi hiyo, bali vijana wapewe nafasi ya kufanya wanachotaka.